Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameionya serikali ya Somalia kuacha uchokozi wa mara kwa mara dhidi ya Kenya.

 

Onyo lake linajiri siku moja baada ya wakazi wa Mandera kulazimishwa kutoroka makazi yao baada ya ghasia zilizozuka kati ya wanajeshi wa Somalia dhidi ya wanajeshi wa eneo la Jubaland katika eneo la Bulla Hawa

Ufyatulianaji mkali wa risasi na milipuko ilionekana kutoka katika eneo hilo la Bulla hawa nchini Somali linalopakana na mji wa Mandera.

''Wanajeshi wa kigeni waliokiuka sheria na kupuuza kabisa sheria za kimataifa na maazimio yalioafikiwa walitekeleza vitendo vya uchokozi na ukatili kwa kuwanyanyasa na kuharibu mali za raia wa Kenya wanaoishi katika mji wa mpakani wa Mandera'' , alisema Uhuru Kenyatta.

''Wacheni uchokozi wa mara kwa mara na badala yake angazieni mambo yenu ya ndani''.

Uhuru amesema kwamba taifa la Somalia linapaswa kuangazia maswala ya raia wake kwa kukabiliana na kuushinda ugaidi ili kuweka amani, usalama na udhibiti katika eneo zima la Afrika mashariki.

"Tuhuma za kila mara zisizo na msingi zinazotolewa na Somalia kwamba Kenya inaingilia mambo yake ya ndani ni mbinu ya Somalia kutaka kuitumia Kenya kama kisingizio '', alisema.

Akiongezea kwamba : Kenya haitakubali kutumika kama sababu ya changamoto zinazoikumba Somalia kisiasa.

Kiongozi huyo ametoa wito kwa Somalia kuacha kampeni hiyo chafu dhidi ya Kenya na badala yake kupeleka nguvu yake katika kutoa uongozi bora kwa watu wake.

Alisema kwamba Kenya imelazimika kuathirika pakubwa kutokana na hatua yake ya kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kuweka amani na usalama katika nchi jirani ya Somalia.

Kiongozi huyo pia amesema kwamba Kenya sasa inaunga mkono wito unaotolewa na Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa kieneo na kimataifa wanaoitaka Somalia kutafuta makubaliano mapana ya kisiasa.

Joto la wasiwasi kati ya Nairobi na Mogadishu limeongezeka katika siku za hivi karibuni huku pande zote mbili zikitoa matamko makali ya kulaumiana kwa kuingia katika himaya ya taifa jingine.

Uhusiano kati ya Mogadishu na Jubaland ni tete
Mapigano hayo ya Somalia ni kisa cha hivi karibuni cha wasiwasi kati ya Mogadishu na serikali zake za kijimbo.

Mamlaka ya Jubaland mnamo mwezi Agosti iliishutumu Mogadishu kwa kuingilia uchaguzi wake na kutaka kumpindua madarakani rais wake Ahmed Madobe ili kuweza kujipatia uwezo wa kulidhibiti jimbo hilo.

Madobe ambaye alichaguliwa kwa muhula mwengine ni mshirika mkubwa wa Kenya ambayo inaiona serikali ya Jubaland kama kizuizi kikuu dhidi ya wapiganaji wa Alshabab ambao wametekeleza mashambulizi chungu nzima nchini Kenya.


Waziri wa ulinzi wa eneo la Jubaland Abdirashid Janan alikamatwa mjini Mogadishu mwezi Agosti mwaka jana akiwa njiani kuelekea Addis Ababa kwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za kibinadamu. Alikuwa amehudumu miezi mitano jela kabla ya kutoroka katika mazingira ya kutatanisha mapema mwaka huu.

Tangu Bw Janan alipowasili Kenya, hali ya taharuki mjini Mandera imekuwa ikitanda na kuwalazimu baadhi ya wakazi kuyakimbia makazi yao wakihofia mapigano kuzuka.

Habari za kuwepo kwa Bwana Janan nchini Kenya zimezidisha uhasama wa kidiplomasia kati ya Mogadishu na Nairobi.

Waziri huyo amekuwa akijificha katika hoteli moja mjini Mandera tangu Januari 30 baada ya kukwepa kutoka jela alikokuwa akizuiliwa na serikali ya Somalia tangu Agosti 31, 2019.

Hofu kati ya mataifa hayo mawili pia iko juu kutokana na madai ya umiliki wa eneo moja lililo katika mpaka wake wa bahari hindi linalodaiwa kuwa na gesi pamoja na mafuta mengi.

Mwezi uliopita serikali ya Kenya ilipuuzilia mbali taarifa ya waziri wa maswala ya kigeni wa Somalia kwamba Kenya ilikuwa inaingilia maswala ya ya ndani ya Somalia.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba huenda hatua ya Kenya ya kumlinda waziri wa ulinzi wa eneo la Jubaland Abdirashid Janan huenda ikachochea uhasama zaidi wa kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili na kulemaza vita dhidi ya wanamgambo wa Al-shabaab.

Mchambuzi wa maswala ya kiusalama George Musamali anasema huenda utawala wa rais Farmajo ukasitisha ushirikiano wake na Kenya katika mikakati ya kupambana na wapiganaji wa Al-shabaab.

Inaaminika pia kwamba viongozi wengi wa Kaskazini mwa Kenya, wakiwemo wale wabunge waliokutana na Rais Farmajo, hawaungi mkono hatua ya serikali ya Kenya ya kumhifadhi na kumlinda Bwana Janan.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh