Na Salma Mkalibala

Katika kukabiliana na changamoto ya kero ya umeme Mkoani Lindi, ambayo inatokana na uchakavu wa miundombinu, Hitlafu katika vikatio vya umeme pamoja na ubovu wa mitambo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanesco mkoani humo limeanza mchakato wa ujenzi wa kituo kidogo cha kupokea umeme kutoka Mtwara katika eneo la Mnazi mmoja na kufanikiwa kubadili nguzo chakavu kwa asilimia themanini.

Akiongea kwa njia ya simu na Safari Redio Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Eng. Johnson Mwigune amesema tayari tanesco mkoani hapo imeshaanza mchakato wa ujenzi wa kituo hiko kidogo cha kupokea umeme ambacho kinatarajiwa kugawa umeme katika wilaya ya Nachingwea, Masasi, Ruangwa, Lindi mjini na vijiji pamoja na maeneo jirani ya Mkoa wa Mtwara na kinatarajiwa kumalizika ujenzi na kuanza matumizi yake mapema mwezi wa Oktoba.

Amesema kituo hiko kitakuwa na laini ya msongo mkubwa wa umeme wa Kilovolts 132 ambayo itakuwa inasaidiana na jenereta kutoka mtwara lenye nguvu ya megawatt 20, ambapo kituo kitakuwa na uwezo wa kupoza umeme kutoka Kilovolts 132 hadi kufikia Kilovolts 33 .

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Eng. Johnson Mwigune

Mwigune amesema miundo mbinu ya umeme mkoani humo imekuwa ikiathiriwa mara kwa mara kutokana na mfumo wa umeme unautumika ambao umeunganishwa moja kwa moja kutoka Mkoani Mtwara na kupelekea kuwa na umbali mrefu wa laini za umeme mbao unatembea zaidi ya kilomita 500, hali inayolilazimu shirika kufanya ukarabati mara kwa mara na kudai kuwa hadi sasa wamefanikiwa kufanya ukarabati wa nguzo na kukata miti kwa asilimia themanini.

Hata hivyo Mwigune amesema shirika linampango wa kuwaleta mafundi kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya kurekebisha mfumo wa vikata umeme kwenye matawi ya laini zinazogawa umeme na muda wowote kuanzia sasa mafundi hao watawasili mkoani hapo.

Akizungumzia juu ya malalamiko ya wananchi ambao wamekuwa wakilalamikia suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara bila ya kupewa taarifa amesema mara nyingi wafanyakazi wa Tanesco wamekuwa wakitoa taarifa kwenye vyombo vya habari, kutuma ujumbe kwenye simu za mkononi kwa namba ambazozimeisajiriwa kwenye mfumo pamoja na kutumia matangazo ya mitaani, lakini amedai kuwa wakati mwingine wanashindwa kutoa taarifa kwa wateja kwa kuwa umeme unakatika kutokana hitlafu za gafla kwenye mitambo.

Shirika la umeme Mkoa wa Lindi limewataka wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho shirika linaendelea na juhudi mbali mbali za kuweza kutatua na kutafuta ufumbuzi wa kero ya umeme mkoani humo.

Hivi karibu Mkuu wa Mkoa Lindi Godfrey Zambi alisema alidhishwi na utendaji kazi wa shirika hilo na kulitaka kuboresha utendaji kazi wake ili kuondoa hadha na hasara kwa wananchi kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh