Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza kuwa wafungwa wote wa kisiasa ambao wamekuwa wakizuiliwa korokoroni nchini humo wataachiliwa huru.

Aidha, amesema kituo hatari cha kuwazuilia wafungwa wa kisiasa ambacho kimekuwa kikitumiwa kuwatesa watuhumiwa pia kitafungwa.

Hailemariam Desalegn amesema kwenye kikao na wanahabari kwamba mashtaka yote dhidi ya wale ambao kesi zao bado hazijamalizika yatafutiliwa mbali.

Ethiopia kwa muda mrefu imetuhumiwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu kwa kuwakamata wapinzani wake kwa wingi na kuwazuilia katika juhudi za kuzima upinzani dhidi ya serikali.

Hata hivyo, hii ndiyo mara ya kwanza kwa serikali kukiri kwamba inawazuilia wafungwa wa kisiasa.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch (HRW) limekuwa likiituhumu serikali kwa kutumia sheria za kukabiliana na ugaidi kuwafunga wapinzani wake.

Shirika la Amnesty International limesema hatua ya leo huenda ikaachilia sura mpya kwa haki za kibinadamu Ethiopia.

Wanaozuiliwa katika magereza na vituo mbalimbali kote nchini humo ni pamoja na wanaharakati wa upinzani kutoka majimbo ya Amhara na Oromia.

Majimbo hayo yalishuhudia maandamano ya kupinga serikali 2015 na 2016.

Kuna piawatu kutoka jimbo la watu wa mataifa ya kusini, na wanahabari ambao wamekuwa wakiikosoa serikali.

Ni vigumu kueleza hasa ni wafungwa wangapi wa kisiasa wanazuiliwa nchini humo, lakini mwandishi wetu anakadiria kwamba kuna takriban watu 1,000 wanaozuiliwa kwa makosa mbalimbali chini ya sheria za kupambana na ugaidi.

Bw Hailemariam amesema kituo kikuu cha kuwazuilia wafungwa cha Maekelawi mjini Addis Ababa ambacho HRW tangu 2013 walidai kimekuwa kikitumia mateso kupata habari kutoka kwa washukiwa kitafungwa.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh