blog category

RAIS KENYATTA AKUTANA NA RAILA ODINGA

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, amekutana na kiongozi wa muungano wa Kisiasa wa CORD, Raila Odinga, katika Ikulu ya Nairobi. Wawili hao walikutana alasiri wakati wa chakula cha mchana kwa heshima ya rais Park Guen-Hye wa Korea Kusini ambaye yuko ziarani nchini Kenya.

Taarifa kutoka kwa msemaji wa Ikulu imesema kuwa baadaye, Kenyatta na Odinga walifanya mkutano uliohudhuriwa pia na naibu wa Rais William Ruto na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang'ula.

Kabla ya mkutano huo, Bwana Odinga alikatiza ziara yake katika kaunti ya Narok ambako alitarajiwa kuhudhuria mazishi, na badala yake akawaambia waombolezaji kiwamba rais Kenyatta alikuwa amempigia simu kutaka wakutane mjini Nairobi.

"Nimepata simu kutoka kwa State House niende nizungumze na Uhuru Kenyatta. Naomba ruhusa yenu kama watu wa Narok niende nizungumze na yeye tukielewana nitawaambia Wakenya, tusipozungumza pia nitawajulisheni," akasema Raila.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alikuwa ameenda kuhudhuria mazishi ya mke wa mwanachama wa kwanza wa seneti baada ya Uhuru Bw Lemein katika kijiji cha Motonyi, kaunti ndogo ya Narok Kaskazini.

Haya yamejiri huku hali ya wasiwasi ikitanda baada ya kiongozi huyo wa upinzani kutangaza kwamba atakaidi amri na kufanya mkutano sambamba na ule wa maadhimisho ya sikukuu ya Madaraka, siku ya Jumatano.

Upinzani umekuwa ukiitisha mkutano wa kujadili maswala ambayo unasema ungependa yashughulikiwa kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao.

Awali, serikali ilitangaza kwamba hakuna mikutano ingefanyika sambamba na ule wa Madaraka, ambao unatarajiwa siku ya Jumatano kwenye uwanja wa Afraha, mjini Nakuru.

Jumanne alasiri, gazeti la Daily Nation liliripoti kwamba Odinga na Kenyatta walikuwa wanaendelea na mkutano wao katika Ikulu.

Picha zilizotolewa na Ikulu ya Nairobi zilimuonyesha Odinga akila chakula cha mchana katika Ikulu na akiketi katikati ya mbunge wa Jubilee Adan Duale na Waziri wa usalama wa ndani, Joseph Nkaisery, ambao wamekuwa wakosoaji wake kwa misimamo yake ya kisiasa.

Kiongozi huyo wa ODM alinukuliwa akisema kwamba ana furaha kwa sababu rais Kenyatta alimpigia simu akitaka mazungumzo na kwamba alitumaini kuwa makubaliano kuhusu maswala nyeti - pamoja na lile la kutaka kuondolewa kwa maafisa wa tume ya uchaguzi kabla ya uchguzi mkuu wa mwaka kesho - yataafikiwa.

Mji wa Mombasa nchini Kenya unatambulika ulimwenguni kote kutokana na mandhari yake yanayowavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali.

Wizara ya utalii ya Kenya imekuwa ikifanya kila juhudi kuhifadhi sifa za mji huo kiutalii ili kukuza sekta ya utalii inayotajwa kuchangia pato kubwa kwa uchumi wa taifa la kenya.

WAFUNGWA JELA MAISHA KWA MAKOSA YA UGAIDI UGANDA

Watu 5 waliopatikana na hatia ya mashtaka ya ugaidi kufuatia shambulio la bomu la mwaka 2010 katika mji mkuu wa Uganda Kampala ambalo liliwaua watu 74 wamepewa hukumu ya kifungo cha maisha jela.

Miongoni mwao ni Issa Ahmed Luyima ,mpangaji mkuu wa mashambulio hayo yaliodaiwa kutekelezwa na kundi la kigaidi la al-Shabab.

Watu wengine wawili waliopatikana na hatia ya ugaidi walipatiwa hukumu ya kifungo cha miaka 50 jela.

Akitoa hukumu hiyo,jaji Alfonse Owiny-Dollo alisema hakuamini kwamba hukumu ya kifo itazuia visa kama hivyo.

Kupatikana kwao na hatia ni mara ya kwanza kwa washukiwa wa kundi la wapiganaji wa al-Shabab nje ya Somalia.

Watu wengine sita ambao pia walishtakiwa waliachiliwa kwa mashtaka ya ugaidi na mauaji ,lakini mmoja wao alipatikana na hatia ya shtaka la kiwango cha chini.

WAHAMIAJI WAPATAO 700 WANAHOFIWA KUFARIKI

Umoja wa mataifa unasema kuwa huenda wahamiaji wapatao 700 wanahofiwa kufariki katika kipindi cha siku tatau zilizopita katika bahari ya Mediterranean.

Msemaji wa Shirika la umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi, Carlotta Sami, amesema kuwa mashua kadhaa yalizama katika maeneo ya kusini mwa Italia Jumatano usiku ikiwa na wahamiaji hao.

Wahamiaji waliokololewa juma lililopita kutoka katika boti moja kwenye bahari ya Mediterranea, wamewaambia wafanyikazi wa makundi ya uokoaji kuwa, waliona chombo kimoja cha baharini kilichojaa wakimbizi kikizama.

Shirika moja la uokoaji la Save the Children, limsema kuwa manusura hao walisema kuwa walingoa nanga katika msafara wa maboti matatu Jumatano usiku kutokea Libya.

Maafisa wa Polisi wa Italia wanasema waliwahoji wahamiaji hao waliofika mjini Sicily hapo Jana Jumamosi.

Juma lililopita pekee, zaidi ya watu 13,000 wameokolewa katika bahari ya Mediterranean.

Mabaki ya ndege ya Eagyptair

Jeshi la Misri na shirika la safari za ndege nchini humo zimesema kuwa mabaki ya ndege ya Egyptair iliotoweka yamepatikana katika bahari ya Mediterenean.

Ndege hiyo aina ya Flight 804 ilikuwa ikielekea kutoka Paris kuelekea Cairo ikiwa na abiria 66 na wafanyikazi wakati ilipotoweka siku ya Alhamisi.

Msemaji wa jeshi la Misri amesema kuwa mabaki na abiria wa ndege hiyo walipatikana kilomita 290 kutoka mji wa Alexandria.

Katika taarifa yake , rais Abdel Fattah al-Sisi alisikitishwa na ajali hiyo.

Kampuni ya ndege ya EgyptAir pia imethibitisha kupatikana kwa mabaki hayo katika mtandao wake wa Twitter.

Mataifa ya Ugiriki, Misri, Ufaransa na Jeshi la Uingereza yamekuwa yakishiriki katika oparesheni ya kuisaka ndege hiyo karibu na kisiwa cha Karpathos.

Ugiriki inasema kuwa rada yake imekuwa ikionyesha kwamba ndege hiyo iligeuka kwa ghafla mara mbili na kuanguka kutoka futi 25,000 na kuingia katika maji.

WHO;KUPAMBANA NA ZIKA

Shirika la afya duniani WHO linasema kuwa limeingilia kati katika kukabiliana na virusi vya Zika huku kukiwa na wito kwa mashindano ya michezo ya Olimpiki kuahirishwa kufuatia mlipuko wa virusi hivyo.

Afisa wa WHO Bruce Aylward amesema kwamba hatua za kukabiliana na ugonjwa huo zimekamilishwa.

Alikiri kwamba shirika la afya duniani WHO linaweza kufanya kazi nzuri zaidi kupitia kutoa tangazo kuhusu kile kinachoendelea na kwamba hakuna haja ya kuahirisha michezo hiyo.

Katika barua ya wazi wanasayansi 152 walisema kuwa utafiti waliofanya kuhusu Zika umeonyesha kuwa ni hatari kwa michezo hiyo kuendelea.

Pia wamesema kuwa shirika hilo la afya duniani linafaa kufuata maelezo yake kuhusu Zika.

Ugonjwa huo unahusishwa na watoto walio na vichwa vidogo na ubongo uliodumaa.

Kati ya Februari na Aprili,Brazil ilisajili zaidi ya visa 90,000 vya Zika.

Visa vya watoto waliohusishwa na virusi hivyo ni 4,908 kufikia mwezi Aprili

Rwanda yawatimua raia wa Burundi

Maafisa nchini Burundi wanasema kwamba Rwanda imewafukuza zaidi ya raia elfu moja mia tatu wa Burundi kutoka nchini humo katika kipindi cha wiki moja iliyopita, baada ya wao kukataa kuhamishiwa hadi katika kambi ya wakimbizi.

Afisa mmoja amesema kuwa wale ambao walikataa kwenda katika kambi ya wakimbizi, walinyanganywa mali yao na kisha wakafukuzwa.

Makumi kwa maelfu ya Warundi walikimbilia Rwanda tangu ghasia zilipoanza nchini mwao mwaka mmoja uliopita, kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuwania Urais kwa muhula wa tatu kinyume na katiba.

Rwanda pia imewatimua Warundi ambao wameishi na kufanya kazi nchini humo kwa miaka mingi.

PUNDA WA VISHWA NEPI KENYA

Kaunti moja ya Kaskazini mashariki mwa Kenya imechukua hatua zisizo za kawaida kulinda barabara moja iliotiwa lami, kwa kuwavalisha nepi punda wanaotumia barabara hiyo.

Mikokoteni yote inayofanya kazi Wajir sasa italazimika kuweka begi nyuma ya wanyama hao ili kuokota kinyesi chao kwa lengo la kuhakikisha barabara iko safi.

Ni barabara kuu ya kwanza katika historia ya eneo hilo.Wakenya wameenda katika mitandao ya kijamii ili kusambaza uvumi vile punda wa Wajir wanapaswa kufuata sheria hiyo mpya mara moja.

Taarifa iliyotolewa na Serikali imesema ''Tunashukuru mchango unaoletwa na waendesha mikokoteni ya punda kwa uchumi wa Wajir,hatahivyo,mji huo ni sharti usafishwe kila mara.Kutokana na hilo,mumeagizwa kusimamia kinyesi cha punda wenu ili kutochafua barabara.Hakuna Punda atakayeruhusiwa mjini bila mfuko wa kubebea kinyesi kufikia tarehe 29 mwezi Mei''.

BUSH;SIMPIGII KURA TRUMP

Aliyekuwa mgombea wa urais wa tiketi ya chama cha Republican nchini Marekani, Jeb Bush, amesema kuwa hatampigia kura Donald Trump katika Uchaguzi wa Novemba.

Bwana Bush alisema kuwa Trump hana tabia wala mienendo ya kuwa Rais wa Marekani.

Jeb ni mojawapo wa wanachama mashuhuri wa Republican kutanganza hadharani kuwa hatompigia kura Bwana Trump kwa sababu ya kampeni yake ya kiburi ambayo imegawanya chama cha Republican.

Mnamo Alhamisi Spika wa Bunge, Paul Ryan, alisema kuwa hatamuunga mkono mfanyabiashara huyo tajiri, ingawa atakutana naye juma lijalo.

Hata hivyo Bwana Trump ameungwa mkono na mgombezi wa Urais wa zamani Bob Dole aliyeshindwa katika uchaguzi na Bill Clinton wa chama cha Democratic mwaka 1996.

Page 101 of 104