blog category

MGOMO WAITIKISA VENEZUELA

Mamilioni ya Wavenezuela wameitikia wito wa Upinzani wa kubakia nyumbani, katika mgomo wa kwanza wa saa 24 kufanyika nchini humo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Hatua hiyo ni kupinga mipango ya serikali ya kuandika tena katiba mpya.

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi katika miji kadhaa, walipopambana na waandamanaji.

Katika ghasia hizo waandamanaji watatu waliuawa.

Hata hivyo, katika maeneo yanayounga mkono serikali ya nchi hiyo mjini Caracas, maisha yaliendelea kama kawaida.

Katika hotuba yake kupitia televisheni, Rais Nicolas Maduro amesema mamia ya wafanyabiashara waliendelea na shughuli zao kama kawaida na kwamba viongozi wa mgomo huo watakamatwa.

Lakini upinzani nao umedai kuwa Rais Maduro anajaribu kujiimarisha madarakani kwa kubadili katiba, hali ambayo itabadili hali ya sasa ya upinzani kudhibiti bunge.

Na katika Umoja wa Mataifa mwanadiplomasia wa Venezuela amejiuzulu katika kupinga hatua zinazochukuliwa na serikali yake.

TRUMP NA PUTIN WAKUTANA KWA SIRI KIKAO CHA G20

Rais wa Marekani Donald Trump alikutana na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin katika mkutano wa pili wa siri ambao haukutajwa ulipofanyika katika kikao cha mkutano wa mataifa ya G20, imebainika.

Walifanya mazungumzo baada ya mkutano wao wa kwanza lakini ukulu ya White House haijatoa maelezo kuhusu kile kilichozungumziwa.

Rais Trump amekana madai ya kufanyika kwa mkutano huo wa siri na Putin na kusema ni ''habari bandia''.

Uhusiano wa viongozi hao wawili unachunguzwa kufuatia madai kwamba kampeni ya Trump ilishirikiana na Urusi.

Wapelelezi wa Urusi wanaamini kwamba Urusi ilimsaidia bwana Trump kushinda uchaguzi wa mwaka jana kitu ambacho Urusi imekana.

Mkutano wa pili ulifanyika wakati wa chakula cha jioni cha viongozi katika kikao hicho cha G20 mjini Hamburg mapema mwezi huu

Rais wa Marekani alikuwa pekee na Putin alikuwa na mkalimani wake huku vyombo vya habari vya Marekani vikisema kuwa mkutano huo ulichukua saa moja.

Madai ya kilichozungumzwa yaliwasilishwa kwa maafisa wa Ikulu ya Whitehouse na bwana Trump mwenyewe kwa kuwa hakukuwa na wasaidizi wakati wa mkutano huo.

MSEMAJI WA MAWAKILI WA TRUMP AJIUZULU

Msemaji wa mawakili wa rais Donald Trump amejiuzulu, kulingana na vyombo vya habari.

Mark Corallo alikuwa msemaji wa Marc Kasowitz ambaye anamtetea Trump katika uchunguzi kuhusu Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani na kumsaidia rais huyo kupata ushindi.

Ripoti zinasema kuwa bwana Corallo alitofautiana na mipango ya mawakili wa Trump kuwadharau na hata kupunguza uwezo wa maafisa wanaoongoza uchunguzi huo.

Hakujakuwa na tamko lolote kutoka kwake ama hata mawakili hao wa Trump.

Bwana Corallo ni mwandani wa wakili wa idara ya haki Robert Mueller ambaye anaongoza uchunguzi huo dhidi ya Urusi na amemsifu hadharani kulingana na mtandao wa politico.

Afisa huyo amekatishwa tamaa na operesheni za mawakili hao mbali na kambi pinzani zilizopo, ripoti hiyo imeongezea.

Bwana Mueller amewaajiri watu maarufu kujiunga na kundi lake, ambalo linachunguza iwapo kulikuwa na ushirikiano wowote kutoka kwa kundi la Trump ambao Urusi na rais Trump amekana kuwepo.

ZAIDI YA TEMBO 45 WADAIWA KUUWAWA DRC, MWAKA HUU

Maafisa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Garamba nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema kuwa Tembo 45 wameuawa tangu mwanzo wa mwaka huu.

Maafisa hao wanasema endapo uhalifu huo utaendelea kukithiri, Tembo huenda wakapotea kabisa katika mbuga hiyo, ambayo ni moja ya maeneo yaliyo na tembo wengi zaidi barani afrika.

Ripoti zinasema Ndovu hao huuawa na makundi ya waasi nchini DRC, wapiganaji wa kundi la waasi wa LRA kutoka Uganda, na waasi wa Sudan Kusini.

OJ SIMPSON AACHILIWA HURU

Mchezaji nyota wa soka la Marekani a pia muigizaji OJ Simpson amesamehewa kifungo chake cha miaka 33, miaka 9 tu baada ya kuingizwa katika Gereza la Nevada.

"Asante!" alisema Mzee huyo mwenye miaka 70, akiinamisha kichwa pale jopo linalohusika na msamaha kwa wafungwa lilipopitisha uamuzi huo wa kumwachia huru ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu wa 2017.

Simpson anatumikia kifungo kutokana na kosa la uvamizi wa kutumia silaha nzito pamoja na makosa mengine 10 aliyoyafanya mwaka 2007 alipovamia Hotel mjini Las Vegas.

Alikuwa pia ameachiwa mwaka 1995 alipokuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe.

Mwaka 2008, miaka 13 kamili baada ya kuondolewa mashitaka ya iliyoitwa 'Kesi ya karne' alikutwa na hatia ya uvamizi wa hotel.

Yeye pamoja na kundi la watu wengine watano walivamia Hotel na kuelekea katika eneo linalotunza vifaa vya michezo, wakakwapua vitu ambavyo alidai vilikuwa vyake kutokana na ushiriki wake michezoni.

Katika harakati za masamaha huu, OJ Simpson aliwaambia maafisa wa jopo la msamaha kuwa vitu alivyovichukua katika uvamizi ule hata hivyo vilikuja kugundulika kuwa vilikuwa vyake.

OJ Simpson alipata umaarufu mkubwa duniani kutokana na kesi iliyokuwa inamkabili ambapo ilidaiwa alimuua aliyekuwa mkewe pamoja na rafiki yake.

MSICHANA ALIYEJIUNGA NA IS AKAMATWA IRAQ

Viongozi wa mashtaka nchini Ujerumani wanachunguza iwapo msichana wa miaka 16 kutoka Ujerumani ni miongoni mwa kundi la washukiwa wa Islamic State waliokamatwa mjini Mosul.

Aliripotiwa kupatikana na vikosi vya kijeshi katika handaki katika mji huo wa Iraq siku ya Alhamisi pamoja na raia wengine 19 wa kigeni.

Maafisa wanajaribu kuthibitisha iwapo ni msichana huyohuyo aliyepotea kutoka mji wa Ujerumani wa Lulsnitz mwaka uliopita.

Serikai ya Iraq imetangaza ushindi dhidi ya IS mjini Mosul ,ijapokuwa vita vinaendelea katika maeneo mengine ya mji huo wa zamani.

Vita hivyo ambavyo vimechukua miaka tisa viliyawacha maeneo makubwa yakiwa yameharibiwa na kuwaua maelefu ya raia huku takriban watu 920,000 wakiwachwa bila makao.

Picha za msichana huyo aliyekamatwa na wanajeshi wa Iraq zilichapishwa na vyombo vya habari vya eneo hilo.

Chombo cha habari cha Ujerumani DPA kiliripoti kuwa kundi hilo la wageni lilikuwa likimiliki silaha na mikanda ya vilipuzi wakati walipokamatwa.

Washukiwa hao wanashirikisha raia watano wa ujerumani , watatu wa Urusi , watatu wa Uturuki na wawili wa Canada.

RIEK MACHAR, ATAKA MAZUNGUMZO MAPYA

Kiongozi wa Sudan Kusini aliye uhamishoni Riek Machar, ametoa wito wa kufanyika mazungumzo mapya ya amani ili kuweza kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Festus Mogae, Rais wa zamani wa Botswana, ambaye sasa anafanya kazi ya upatanishi, Sudan kusini amemtaka Riek Machar kutangaza kusimamisha mapigano, wakati alipomtembelea kwenye makazi yake ya uhamishoni Afrika kusini.

Amesema Bwana Machar ametaka kufanyika kwa mazungumzo mapya nje ya Sudan Kusini.

Sudan kusini ilijikuta katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumuondosha msaidizi wake Riek Machar

WAASI WAHUSISHWA MAUAJI YA WACHUNGUZI WA UN, DRC

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa huenda wanajeshi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo au wapiganaji wa waasi nchini humo walihusika na mauaji ya wenzao wawili.

Michael Sharp, raia wa Marekani na Zaida Catalan, mwenye uraia wa Uswizi na Chile waliuawa Machi mwaka huu walipokuwa wakifanya utafiti kuhusu hali ya usalama nchini Congo.

Wachunguzi wanasema wenzao hao walipanga kukutana na kiongozi wa wanamgambo, siku moja kabla ya kuuawa.

Page 1 of 83