Idara ya uhamiaji mkoa wa Mtwara imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 18 ambao ni raia wa nchini Ethiopia wakiwa katika harakati za kuvuka katika mpaka wa Kilambo, halmashauri ya wilaya ya Mtwara kuelekea nchini Msumbiji.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, naibu kamishina wa Uhamiaji, afisa uhamiaji mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama, amesema wahamiaji hao wamekamatwa huku ikiwa haijafahamika aliyehusika katika kuwasafirisha, na kwamba leo watafikishwa mahakamani baada ya kujiridhisha kuwa wameingia nchini visivyo halali.

“Sisi kama Uhamiaji ambao ndio jukumu letu kuwashughulikia watu wa aina hii, tuko nao hapa na baada ya muda mfupi tutawafikisha mahakamani baada ya kujiridhisha kwamba wameingia nchini visivyo halali, wamekiuka sheria ya uhamiaji ya kuwapo nchini bila vibali. Lakini kama haitoshi waliweza kupita njia zisizo rasmi..” alisema.

Aidha, alikiri kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya kutumika kama njia kwa wahamiaji, kutokana na kupakana na nchi ya Msumbiji, na kuwataka wananchi kushirikiana na maafisa uhamiaji katika kutoa taarifa za raia hao, ili kukabiliana na changamoto hiyo. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki mbili baada ya waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa, kutoa msisitizo kwa Idara hiyo kuhakikisha inaimarisha ulinzi katika mipaka yote inayopakana na nchi jirani ili kudhibiti raia hao.

Mkoa wa Mtwara umefanikiwa kuwakamata jumla ya wahamiaji haramu 123 kuanzia mwezi Januari mpaka Juni mwaka huu, kutoka katika mataifa Kumi na Mbili na kati ya hao, raia Hamsini na sita ni kutoka nchini Ethiopia.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh