Rais Dkt John Pombe magufuli amempongeza Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako kufuatia kuwatimua wanafunzi 7000 wa ualimu wasiokuwa na sifa za kusoma chuo Kikuu kutoka chuo Kikuu cha Dodoma na wanafunzi 481 kutoka chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Arusha.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa Ujenzi wa Maktaba ya Kisasa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Rais Magufuli amesema ni lazima wanafunzi wanaokwenda chuo kikuu kusomea fani mbalimbali lazima wawe na sifa pamoja na vigezo vya kusoma Chuo kikuu.

Amesema lengo la kuanzishwa kwa kozi hiyo maalumu ya ualimu ilikuwa kwa wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili lakini cha kushangaza Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) ilipitisha wanafunzi wasiokuwa na sifa ikiwemo waliopata daraja la nne na la tatu.

Baadhi ya wanafunzi waliopitishwa Rais Magufuli amesema ni wale watoto wa vigogo ambao miongoni mwao ni wale wasiokuwa na sifa za kusomea chuo kikuu.

Hata hivyo amesema kati ya wanafunzi waliosimamishwa wale waliofaulu vizuri kwa daraja la kwanza na la pili serikali itaangalia namna ya kuwasaidia.

Naye Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es salaam Rais mstaafu Dkt Jakaya Kikwete amesema Chuo Kikuu cha Dar es salaam kina matatizo mengi ikiwemo uhaba wa mabweni ya wanafunzi ambapo asilimia kubwa ya wanafunzi wanaishi nje ya Chuo suala ambalo ni hatari wa mustakabali wa taaluma yao.

Akijibu baadhi ya kero hizo Rais Magufuli amesema atatoa bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na kuitaka mifuko ya jamii kujitokeza kwa wingi katika kufanya uwekezaji wa mabweni kwa kuwa wateja ambao ni wanafunzi wapo wengi.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh