Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), imepongezwa kwa kazi zake inazofanya za utafiti na kutoa mwelekeo sahihi wa uanazuoni kwenye masuala mazito yanayotakiwa kutekelezwa na wananchi wa Tanzania kuendeleza ustawi na kuinua uchumi.

Aidha imepongezwa kwa kurejea kuipitia sera ya maendeleo endelevu (SIDP) ya mwaka 1996 ambayo kwa sasa inahitaji kufanyiwa marekebisho kuendena na maizngira ya sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof Elisante Ole Gabriel, katika hotuba iliyosomwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda wa Wizara hiyo, Obadiah Nyagiro wakati akifungua mkutano wa tano wa wajumbe wa kitaifa wakiwemo wataalamu wa kupitia sera na maeneo maalumu yanayogusa maendeleo (NRG5) ambapo walijadili sera ya maendeleo endelevu ya viwanda: Nini Nafasi ya usalama wa chakula, hali ya hewa na biashara?

Amesema kwamba majadiliano hayo yanakwenda sawa na juhudi za serikali ya awamu ya tano ya kujikita katika maendeleo ya viwanda ambapo uwekezaji na biashara ni vitu muhimu.

Amesema mwaka 1996 serikali ya Tanzania ilizindua sera ya maendeleo endelevu (SIDP) ikiwa imepangwa kuibeba nchi kuanzia mwaka huo hadi mwaka 2020.

Lengo ya sera hiyo ni ilikuwa kuiweka Tanzania katika njia ya viwanda na kufikia malengo ya kitaifa kama ilivyoelezwa katika malengo ya taifa (TDV) kufikia 2025.

Alisema kwa miaka mingi utekelezaji wa SIDP umekuwa ukisaidiwa na sera mbalimbali za kilimo, fedha na biashara na mikakati ya maendeleo.

Kuelekea katika viwanda kunakwenda sanjari na kuangalia mipango ya maendeleo ingawa kuna hisia kwamba suala la usalama wa chakula mabadiliko ya hali ya hewa na usindikaji wa mazao ya kilimo yamekuwa yakiachwa katika kuongeza uimara wa safari ya maendeleo.

Mapungufu yaliyopo ndani ya SIDP yanahitaji kuangaliwa ili kutoa umuhimu wa kuunganisha masuala hayo muhimu ambayo ni mtambuka na maendeleo ya viwanda.

Kwa kuunganisha masuala hayo na kuangalia jinsia taifa litakuwa na sera bora kabisa ya viwanda yenye kubeba kila kitu kinachotakiwa katika kuelekea uchumi unaotegemea viwanda na kujali mazingira.

Amesema kutokana na mazingira hayo ni dhahiri kwamba mkutano huo na maazimio yake yatakuwa chachu kwa watengeneza sera ambao wanatakiwa kuipitia sera hiyo na kuipa uhai mpya.

Naye Mkuu wa Idara ya Utafiti na Machapisho wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene aliyesoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dk Tausi Kida akikaribisha wajumbe wa mkutano huo, alisema kwamba mkutano huo mkubwa wa kitaifa umelenga kutoka na maazimio ambayo yatasaidia watunga sera kuihuisha sera iliyopo na mikakati mbalimbali ya kuipeleka Tanzania katika dunia ya viwanda.

Alisema mkutano huo unafanana na ule uliofanyika Agosti 24 mwaka jana ambao uliangalia mambo mbalimbali yanayohusiana na sera hiyo na kuihusisha katika SIDP.

Alisema haja ya kuangalia sera hiyo kunatokana na ukweli kuwa kuna mapengo kadha katika sera yanayosababisha ufanisi mdogo wenye tija katika uchumi na biashara pia katika kilimo.

Upitiaji huo wa SIDP umefanywa na ESRF kwa kufadhiliwa na CUTS International na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Washiriki pia walipata nafasi ya kupewa taarifa ya hali ya kilimo nchini na majadiliano ya masoko kupitia Shirika la Biashara Duniani (WTO) na taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia na mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC).

Katika mkutano huo mada mbalimbali ziliwasilishwa zilizoangalia sekta mtambuka zikiwamo za kilimo na viwanda.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh