Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameuagiza Uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), kuanza mara moja mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa Mtaa wa Nyamalembo mjini Geita, ambao nyumba zao zimeathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi huo.

Aidha, Naibu Waziri ameutaka Mgodi huo kuchagua moja kati ya kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Nyakabale ambacho kipo ndani ya eneo la Leseni yao, ili waondoke au kutoa tamko la kuwaruhusu kuendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika eneo hilo.

Nyongo ametoa maagizo hayo Februari 23 na 24 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Geita, ambapo alikutana na wananchi wa maeneo husika kujionea hali halisi, kuzungumza nao na kisha kukutana na uongozi wa GGM.

Nyongo alisema anatambua kuwa GGM wanatumia kigezo cha sheria na kanuni inayowaruhusu kutolipa fidia ya ardhi katika maeneo ambayo bado hawajaanza kuyafanyia kazi, lakini hata hivyo aliwataka kutumia kigezo cha ubinadamu na uhusiano mwema kuwalipa wananchi hao.

Alitahadharisha kwamba, yawezekana kukawa na udhaifu au upungufu katika sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza sekta husika, na kwamba wako baadhi ya watu wanaotumia mwanya huo kuwakandamiza wengine, hususan wananchi.

Naibu Waziri Nyongo alisema Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi makini wa Rais Dkt. John Magufuli, haiwezi kukubali kuona mwekezaji yeyote anakuwa kero kwa wananchi.

Akizungumzia umuhimu wa kujenga uhusiano mzuri na amani ya kudumu baina ya wawekezaji na jamii inayowazunguka, Nyongo alisema kuwa suala hilo linawezekana endapo kutakuwa na utaratibu wa mazungumzo na makubaliano ya masuala mbalimbali kati ya pande zote husika.

Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa lengo la Serikali siyo kuwafukuza wawekezaji bali ni kuhakikisha wanafanya kazi yao ya uwekezaji pasipo kuwakandamiza wananchi.

Alisema kuwa, ni lazima pande zote mbili zihakikishe zinafuata sheria na taratibu zilizowekwa, lakini wasisahau kujenga mahusiano mazuri baina yao.

Akizungumzia tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya leseni za wawekezaji wakubwa, Nyongo alisema kuwa siyo sahihi na kuwataka kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha Kamisheni maalum itakayoshughulikia sekta ya madini, na kwamba inatarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni. Aliwataka wachimbaji wadogo wasio na leseni wahakikishe wanafuata taratibu husika mara tu Kamisheni hiyo itakapoanza kufanya kazi ili wapate leseni na kurasimishwa katika kazi hiyo.

Alisema kuwa, Serikali inataka kuona wachimbaji wote wa madini wanafanya kazi zao kwa amani ili walipe kodi na tozo zote stahiki ili kuwezesha kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliuagiza Mgodi wa GGM kuzingatia umuhimu wa kuwawezesha wananchi wanaowazunguka na Taifa kwa ujumla kwa kutumia na kutoa kipaumbele kwa bidhaa na huduma zinazopatikana ndani ya nchi na maeneo ya jirani kwani suala hilo lipo kisheria.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh