Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Elius Mwakalinga akafanye tathmini ya ubora ya jengo la kituo cha pamoja cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.

Ametoa agizo hilo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo alimuagiza Mkurugenzi huyo afanye tathmini na kuishauri Serikali kama jengo linafaa kutumika.

Januari 17, 2018 Waziri Mkuu alikagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo alisema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango.

Pia Waziri Mkuu alipokagua jengo hilo alijionea mwenyewe kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu miradi ya maji inayotekelezwa katika mkoa huo, ambapo alisema “Miradi mingi ya maji mkoani Mara ni ya hovyo na fedha nyingi zimetumika na wananchi hawajapata huduma hiyo.”

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaelekeza viongozi wa mkoa huo ifikapo Januari 25, 2018 wamkabidhi taarifa ya mikakati waliyonayo ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh