Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi leo Januari 23.2018, kwenye uzinduzi wa Onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika, tukio ambalo litafanyika majira ya saa 11 jioni katika viunga vya Makumbusho ya Taifa, yaliyopo mtaa wa Shabani Robert, mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Akizungumza wakati wa utambulisho wa tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla amebainisha kuwa, tayari maandalizi ya onesho hilo yameenda sawa na watu mbalimbali watanatarajiwa kushuhudia tukio ambalo ni la siku moja wakiwemo viongozi wa Serikali na Mabalozi waliopo nchini, na watalii wanatarajiwa kuhudhuria.

Profesa Mabulla amebainisha kuwa, Vioneshwa vyote katika onesho hilo hapo kesho, vimepatikana hapa Tanzania kutokana na tafiti za kisayansi na vimehifadhiwa Makumbusho ya Taifa.

Kwa upande wake Mratibu kwa upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna amesema Onesho limegawanyika katika sehemu kuu nne zikiwemo Makumbusho ya Taifa la Tanzania ikishirikiana na Ubalozi wa Spain Tanzania.

Hii ni pamoja na Makumbusho ya Akiolojia ya Madrid, Taasisi ya Chimbuko la Binadamu (IDEA) Madrid, Chuo Kikuu cha Alcala Madrid na Makumbusho ya CosmoCaixa Barcelona-Spain huku tamasha zima likidhaminiwa na Kampuni ya Simenti ya Twiga.

Aidha Dk.Agness ameongeza kuwa, Onesho hilo litakuwa katika pande nne ikiwemo sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dkt. Mary D. Leakey. Nyayo hizo ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ni ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopia.

Sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo) ambapo kuna masalia ya zamadamu Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo (Oldowan) zilizotumika katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.

Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus. Jamaii hii inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kuna masalia ya zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile tembo na nyati wa zamani takribani miaka million 1.7 iliyopita.

Sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Kuna masalia ya Homo sapiens na zana za mawe za muhula wa kati na muhula wa mwisho.

Mbali na onesho hilo, pia waandaji hao wa Makumbusho ya Taifa inawakaribisha watu wote kuhudhuria semina na ufunguzi wa onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh