Wakazi wa Kata ya Kinyerezi eneo la Kifuru kwa Kinana wameulalamikia uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kituo cha Tabata jijini Dar es Salaam kwa kitendo cha kutelekeza nguzo na nyaya za mradi wa umeme eneo hilo ambapo zimegeuka kero.

Wakizungumza eneo hilo kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wakazi hao, wamesema TANESCO kituo cha Tabata walileta nguzo na nyaya tangu mwaka jana na kuziweka barabara inayoelekea King’azi (Kwa Godoro) Mtaa wa Tanganyika ambapo baada ya mvua za mwishoni mwa mwaka jana 2017 baadhi ya nguzo zilianguka na nyaya kutandaa chini jambo ambalo limekuwa kero baada ya kuziba barabara ya mtaa huo na magari kupita kwa taabu.

Mkazi wa Mtaa wa Tanganyika, Rashid Abdallah alisema mradi huo umechukua zaidi ya miaka miwili sasa huku wateja walioomba umeme eneo hilo wamekuwa wakizungushwa kwamba wasubiri mradi huo bila ya mafanikio.

Alisema kwa sasa wamekuwa kama walinzi wa nguzo na nyaya hizo za TANESCO mtaani hapo maana wanahofia zikiibiwa huenda matumaini ya mradi huo wanaoahidiwa kila kukicha kukamilika ukatoweka kabisa.

Kwa upande wake mkazi mwingine wa eneo hilo, Senzekwa Magila alisema wanashangaa kuzungushwa maombi yao ya kufungiwa umeme wakielezwa kusubiri mradi ambao haukamiliki ilhali wanaendelea kutaabika. Alisema TANESCO inapaswakujifunza na kuwa makini kwa uongozi wa sasa kwani unahimiza uchapaji kazi bora unaolenga kuiingizia Serikali na taasisi zake mapato ya kutosha, jambo ambalo wanashangaa wateja wanaomba huduma zaidi ya miaka miwili bila mafanikio.

Naye mkazi mwingine ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kinachowakaza zaidi ni kitendo cha maeneo yote yaliozunguka mtaa huo kuunganishwa umeme lakini wao Mtaa wa Tanganyika hadi leo wamekuwa wakipigwa danadana bila mafanikio.

Alisema wengi wao wamejinyima na kuanza kufunga mfumo wa umeme mapema katika nyumba zao lakini hadi leo hawajaunganishwa.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh