Wafugaji wilayani Longido Mkoani Arusha wameanza kunufaika na ujenzi wa soko la kisasa la mifugo linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Worendeke kata ya Kimokouwa, kupitia mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB

Baadhi ya wafugaji wamesema kuwa Soko hilo linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 650, limewaondolea adha kubwa waliyokuwa wakiipata walipokuwa wakiuza mifugo yao nchini Kenya kutokana na gharama kubwa ya kusafirisha mifugo kwenda huko pamoja na kulipa kodi na ushuru mbalimbali.

Wamesema kuwa kujengwa kwa somo hilo ni mkombozi mkubwa kwao na kwamba hali hiyo itasisimua uchumi wao kwa kuwa wafanyabiashara wa ndani na kutoka Kenya wamekuwa wakiwafuata kwenye soko hilo kununua mifugo yao hatua inayowafanya wapate faida kubwa.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Bw. Toba Nguvila, amesema kuwa soko hilo ambalo ujenzi wa miundombinu yake umekamilika kwa asilimia 85 limeanza kuiingiza Serikali mapato yake ambapo kwa wastani Halmashauri ya wilaya inakusanya wastani wa shilingi milioni 1 kwa siku.

“Asilimia 95 ya wakazi wa wilaya yetu ni wafugaji wa kimaasai ambao kwa kipindi kirefu wameteseka kusafirisha mifugo yao kwenda Kenya na kutopata faida kutokana na gharama kubwa ya kusafirisha, kupitisha mifugo kwenye maeneo ya watu hivyo kulazimika kulipa ushuru, halikadhalika kulipia tozo mbalimbali wakati wakisubiri kuuza mifugo yao,” alieleza Nguvila

Alisema kuwa kuanzishwa kwa soko hilo litakalokuwa na miundombinu muhimu kama vile mizani ya kupimia uzito wa mifugo yao kabla ya kuiuza, si tu kwamba limesababisha wafugaji kupata faida kwa kuuza mifugo yao kwa bei nzuri ya soko, bali pia limeleta neema kwa wafanyabiashara wengine wadogo wakiwemo mamalishe.

Akina mama wanaofanya biashara zao za kuuza chai na chakula huku kundi kubwa la vijana waliokuwa wakiuza bidhaa zao za kutembeza mikononi katika mpaka wa Kenya na Tanzania-Namanga, ambao wamejiajiri kwa shughuli za kushusha na kupakia mifugo kwenye malori,” aliongeza Nguvila

Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa mifugo inaongezewa thamani, mchakato wa kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata mifugo 3,000 kwa siku kinatarajiwa kujengwa katika eneo la karibu na soko hilo kwa ajili ya kuuza nyama ndani na nje ya nchi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayesimamia nchi 7 za Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, amesema Benki yake imefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko hilo litakalochochea uchumi wa wananchi.

Ameahidi kuwa Benki yake inafadhili ujenzi wa masoko mengi ya namna hiyo hapa nchini na nchini nyingine za Kiafrika ili nchi hizo ziweze kukuza uchumi wake na maisha ya watu wake kwa ujumla.

“Benki iko tayari kuendelea kusaidia eneo hili la ujenzi wa masoko ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi hivyo naushukuru uongozi wa mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido kwa kazi nzuri wanayoifanya kusimamia ujenzi wa soko hili na kwamba ujenzi wake utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa,” alisisitiza Dkt. Weggoro.

Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB inafadhili ujenzi wa masoko kadhaa Tanzania Bara na Visiwani kupitia mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 56 na unatekelezwa kupitia mpango wa kuendeleza miundombinu ya masoko, kuongeza thamani ya mazao na uboreshaji wa huduma za kifedha vjijini.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh