Taasisi ya Bill and Mellinda Gates imetenga Dola za Marekani Milioni 350 sawa na takribani Shilingi za tanzania Bilioni 777.084 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.

Mwenyekiti Mwenza wa Taasisi hiyo Bill Gates amesema hayo Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambapo amesema, fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na utapiamlo, na kwenye sekta ya kilimo ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula.

Rais Magufuli amemshukuru Bill Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na taasisi ya Bill and Mellinda Gates katika miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo fedha itakazotoa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa ambapo amemhakikishia kuwa Serikali itahakikisha zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Inmi Patterson ambaye amesema Marekani itatoa fedha za nyongeza kiasi cha Dola Milioni 225 sawa na Shilingi Bilioni 499.500 za Tanzania katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora.

Rais Magufuli amemshukuru Balozi Inmi Patterson kwa mchango mkubwa ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali yake itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Marekani, na amemuomba awahamasishe wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa Marekani waje kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini kutokana na fursa zilizopo.

Aidha ameiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya kitaifa katika makao makuu ya nchi Dodoma ili kuongeza uwezo wa Mkoa huo kutoa huduma za matibabu.

0768671579

Add comment


Security code
Refresh