blog category

SERIKALI YA YACHACHAMAA SUALA LA NGUVU ZA KIUME

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile ametaja sababu za Serikali kufanya utafiti wa tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume kuwa linatokana na baadhi ya waathirika kutafuta suluhisho la tatizo hilo kinyemela na hivyo kukosekana taarifa sahihi.

Dk Ndugulile amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya utafiti wa afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu na pia kujua ongezeko la upungufu wa nguvu za kiume ni kubwa kwa kiasi gani nchini.

Dk Ndugulile amesema kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikitilia mkazo afya ya uzazi kwa wanawake na tafiti nyingi zimekuwa zikihusu upande huo mmoja.

Amesema mpaka sasa bado haujafanyika utafiti kuhusu hali ya afya ya uzazi kwa wanaume, japokuwa tatizo hilo linazungumzwa miongoni mwa wanajamii.

Hata hivyo, alisema takwimu za sayansi duniani zinaonyesha kuwa wanaume wengi wana matatizo ya nguvu za kiume, sababu kubwa ikiwa ni mtindo wa maisha.

Wakati huo Wizara ya Afya jana ikitangaza kuzisajili dawa tano za asili ikiwamo ya Ujana iliyothibitishwa kutibu tatizo la upungufu wa nguvu za kiume, imebainika kuwa zipo dawa ambazo si za asili za kutibu tatizo hilo katika maduka ya dawa.

Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza amesema dawa ambazo zimesajiliwa baada ya kuchunguzwa na kuonekana zinafaa kutumiwa na binadamu ni za aina mbili, “Sildenafil pamoja na Tadalafil zinazotoka nchi za nje, zimechunguzwa na TFDA na kuonekana hazina sumu wala madhara kwa watumiaji, hizi zinapatikana maduka mbalimbali ya dawa za binadamu,” alisema Simwanza.

Utafiti uliofanywa na daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Henry Mwakyoma aliwahi kufanya utafiti kuhusu ukosefu wa nguvu za kiume na ugumba.

Alisema, ukosefu wa nguvu za kiume ni kukosa uwezo wa kufanya tendo la ndoa na ugumba ni uwezo hafifu wa mbegu za mwanamume kuzalisha.

KWA KHERI HASSAN ISSA SIMBA

Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwa na umoja hususani wanapo patwa na matatizo ili kuweza kulinda tasnia hiyo na kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni (mstaafu) Mhe. George Mkuchika (Mb) wakati akitoa salamu za pole kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mtwara , katika mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa  huo Hassan Simba yaliyo fanyika katika kijiji cha Tingi kilichopo wilayani Kilwa.

Mh Mkuchika amemuelezea Simba kuwa ni kielelezo na Mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari na wanahabari wanakila sababu ya kuiga mazuri aliyo yaacha.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa vyama vya waandishi wa Habari nchini Christopher Lilahi amesema kuwa imefika wakati kwa sasa kwa wanahabari kuwa na bima za afya ili inapo tokea ugongwa iwe rahisi kupata matibabu

Hassan Issa Simba amezaliwa mwaka 1970 na amefikwa na umauti februari 24 mwaka huu wa 2018

Bwana ametoa ,Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.

UN WAINGIA MAKUBALIANO NA SERIKALI KUTANGAZA MPANGO WA MAENDELEO

Umoja wa Mataifa umeingia makubaliano ya kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa habari za maendeleo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO).

Makubaliano hayo yamelenga kuimarisha upatikanaji na utoaji habari wa pamoja kuhusu mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa serikali na malengo ya maendeleo endelevu ya dunia.

Kwa mujibu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Bw. Alvaro Rodriguez makubaliano hayo yatachagiza kupatikana kwa habari kuhusiana na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu unaokwenda sambamba na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa Tanzania.

Akizungumzia malengo hayo kwa maofisa wa mawasiliano wa serikali wanaokutana mjini Arusha kwa semina ya wiki moja iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya TAGCO na Wizara ya Habari na kufadhiliwa na Umoja wa Mataifa, alisisitiza kuwa malengo hayo yanahitaji kuwasilishwa kwa wananchi na pia kupigiwa chapuo.

Amewataka maofisa mawasiliano hao wa serikali kufanyakazi ya uragibishi na pia kuwasiliana ana kwa ana na jamii kuhusu masuala mtambuka kama kuhifadhi mazingira,kuondoa tatizo la ukeketaji (FGM) na kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika kufanikisha mpango wa maendeleo wa kitaifa na ule wa dunia.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Maelezo Dk. Hassan Abbas alisema kwamba kwa sasa wizara ya habari iko katika mchakato wa kuandaa makubaliano na Umoja wa Mataifa yatakayogusa masuala ya mawasiliano katika utekelezaji wa mpango wa pili wa miaka mitano wa maendeleo m na malengo ya maendeleo endelevu ya dunia.

Aidha alisema semina hiyo itawapatia mafunzo mengi maofisa hao ikiwa ni pamoja na kutembelea maeneo yenye miradi iliyopata mafanikio na kujenga athari chanya kwa jamii.

MBUNGE WA MBEYA JOSEPH MBILINYI AFUNGWA JELA KWA KUMTUSI RAIS MAGUFULI

Mbunge wa Mbeya mjini kwa tiketi ya Chadema Joseph Haule Mbilinyi kwa jina maarufu Sugu na mwenzake Katibu wa Chadema Kanda ya nyanda za juu kusini, Emmanuel Masonga wamehukumiwa kufungwa jela miezi mitano.

Wawili hao walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mwezi Desemba mwaka jana jijini Mbeya.

Hukumu dhidi yao imetolewa na Mahakama ya hakimu mkazi jijini Mbeya.

WAZIRI MWIJAGE AKIRI KUCHUKIZWA

Waziri wa Viwanda, Biashara na uwekezaji Charles Mwijage amesema kuwa hapendezwi na bei elekezi za sukari zilizopo kwa sasa na anajitahidi kutengeneza viwanda vidogo vya sukari kama 100 ili soko la sukari lijiendeshe lenyewe.

Amesema hayo katika ziara yake ya kushtukiza mkoani Manyara na kuweza kutembelea kiwanda kidogo cha sukari cha Manyara Sugar na kuona uzalishaji uliopo na kusema kuwa kupanda kwa bei nikutokana na viwanda vingi kufungwa lakini serikali imetoa vibali vya kuagiza tani mia moja thelathini elfu na kwa sasa zimeshaanza kuingia na mpaka mwezi wa sita zitazuiliwa ikiwa tayari viwanda vya ndani vitaanza kusambaza sukari hiyo.

Pamoja na hayo Waziri Mwijage amefungua eneo maalumu la ujenzi wa viwanda ambalo linaukubwa wa ekari 9.14 ambapo ekari 6.855 litajengwa majengo matatu ambayo yataanzishwa viwanda kumi vidogo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Manyara Sugar BW. Bharabat Sesodya amesema kuwa kutotosheleza kwa sukari ni kutokana na udogo wa uzalishaji lakini kwa sababu mwaka huu wanamiwa ya kutosha lazima wafikie lile lengo la serikali lililo kusudia.

GGM YATAKIWA KUWALIPA FIDIA WANANCHI

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameuagiza Uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), kuanza mara moja mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa Mtaa wa Nyamalembo mjini Geita, ambao nyumba zao zimeathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi huo.

Aidha, Naibu Waziri ameutaka Mgodi huo kuchagua moja kati ya kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Nyakabale ambacho kipo ndani ya eneo la Leseni yao, ili waondoke au kutoa tamko la kuwaruhusu kuendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika eneo hilo.

Nyongo ametoa maagizo hayo Februari 23 na 24 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Geita, ambapo alikutana na wananchi wa maeneo husika kujionea hali halisi, kuzungumza nao na kisha kukutana na uongozi wa GGM.

Nyongo alisema anatambua kuwa GGM wanatumia kigezo cha sheria na kanuni inayowaruhusu kutolipa fidia ya ardhi katika maeneo ambayo bado hawajaanza kuyafanyia kazi, lakini hata hivyo aliwataka kutumia kigezo cha ubinadamu na uhusiano mwema kuwalipa wananchi hao.

Alitahadharisha kwamba, yawezekana kukawa na udhaifu au upungufu katika sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza sekta husika, na kwamba wako baadhi ya watu wanaotumia mwanya huo kuwakandamiza wengine, hususan wananchi.

Naibu Waziri Nyongo alisema Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi makini wa Rais Dkt. John Magufuli, haiwezi kukubali kuona mwekezaji yeyote anakuwa kero kwa wananchi.

Akizungumzia umuhimu wa kujenga uhusiano mzuri na amani ya kudumu baina ya wawekezaji na jamii inayowazunguka, Nyongo alisema kuwa suala hilo linawezekana endapo kutakuwa na utaratibu wa mazungumzo na makubaliano ya masuala mbalimbali kati ya pande zote husika.

Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa lengo la Serikali siyo kuwafukuza wawekezaji bali ni kuhakikisha wanafanya kazi yao ya uwekezaji pasipo kuwakandamiza wananchi.

Alisema kuwa, ni lazima pande zote mbili zihakikishe zinafuata sheria na taratibu zilizowekwa, lakini wasisahau kujenga mahusiano mazuri baina yao.

Akizungumzia tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya leseni za wawekezaji wakubwa, Nyongo alisema kuwa siyo sahihi na kuwataka kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha Kamisheni maalum itakayoshughulikia sekta ya madini, na kwamba inatarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni. Aliwataka wachimbaji wadogo wasio na leseni wahakikishe wanafuata taratibu husika mara tu Kamisheni hiyo itakapoanza kufanya kazi ili wapate leseni na kurasimishwa katika kazi hiyo.

Alisema kuwa, Serikali inataka kuona wachimbaji wote wa madini wanafanya kazi zao kwa amani ili walipe kodi na tozo zote stahiki ili kuwezesha kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliuagiza Mgodi wa GGM kuzingatia umuhimu wa kuwawezesha wananchi wanaowazunguka na Taifa kwa ujumla kwa kutumia na kutoa kipaumbele kwa bidhaa na huduma zinazopatikana ndani ya nchi na maeneo ya jirani kwani suala hilo lipo kisheria.

HAWA WATU HAWAMUOGOPI MUNGU - PROF TIBAIJUKA

Mbunge wa Muleba Kusini(CCM), Anna Tibaijuka amesema kuwa wapo watu ndani ya Serikali ya awamu ya tano hawamuogopi Mungu ndiyo maana wanakuwa wanawaonea wananchi na kuichafua serikali pamoja na Rais Magufuli.

Tibaijuka amesema hayo wakati akiongea na wananchi pembezoni mwa mkutano wa hadhara baadaa ya kuona watu wakilipishwa kodi na kupewa risiti za mwaka 2015 fedha ambazo zinaonekana hazifiki serikalini.

Amesema kuwa Serikali ya Rais Magufuli haiwezi kukubali haya mambo wanataka tu kuchafua jina la Rais.

Aidha Tibaijuka amesema kuwa yeye anaamini kuwa Rais Magufuli hawezi kutuma watu kwenda kuchoma nyavu za wavuvi

MUHIMBILI YAFANYA MAAJABU KWA WATOTO SITA

Hospitali ya Taifa Muhimbili imewawashia vifaa vya usikivu watoto sita waliofanyiwa upasuaji maalumu wa kupandikiza vifaa vya usikivu, hatua ambayo hii imewawezesha watoto hao kwa mara ya kwanza kusikia sauti tangia wazaliwe.

Daktari wa upasuaji Pua, Koo na Masikio Dkt. Edwin Liyombo, amesema kuwashwa kwa vifaa hivyo kunaifanya hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa na uwezo wa kufanya upasuaji wa kupandikisha vifaa vya usikivu, upasuaji ambao umekuwa unafanyika nje ya nchi tena kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni inayotengeneza vifaa hivyo ambaye pia ni daktari bingwa wa masuala ya sauti na upandikizaji vifaa vya usikuvu Dkt. Fayaz Jaffer, amesema itachukua takribani mwaka mmoja hadi watoto hao waweze kuzungumza ipasavyo.

Page 2 of 168