blog category

WAKALA WA MAJENGO (TBA) WATEMA CHECHE

Katibu Mkuu Ofisi ya Ras Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe amesema kuwa zaidi ya kaya 438 za watumishi wa umma watakaohamia Dodoma na wenye sifa ya kupatiwa nyumba na Serikali 2watakuwa na uhakika wa kupata nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)

Akikabidhi Nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kwa Wakala wa Majengo (TBA) Mhandisi Mussa Iyombe amesema, nyumba hizo zitakuwa maalum kwa watumishi wenye sifa kulingana na miundo ya kitumishi.

Akitoa Maelezo ya awali Mhandisi Musa Iyombe amesema baada ya kuivunjwa kwa CDA iliagizwa kuwa watumishi wote waliokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kupangiwa kazi kwenye Ofisi za Serikali na kipaombele cha kwanza kilikuwa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuchagua watumishi wanaomfaa kwa ajili ya kuendeleza kazi zilizokuwa zikifanywa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kazi ambayo kwa sasa imekamilika.

Mhandisi Iyombe amesema mali zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yakiwemo majengo ya kibiashara kama vile maduka na ofisi zimeelekezwa zibaki chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lakini majengo ya makazi yakabidhiwe kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

Akifafanua zaidi Mhandisi Iyombe amesema majengo yaliyopo ni 141 kati ya hayo kuna magorofa 45 hivyo familia ambazo zinaweza kuingia katika majengo hayo ni kaya 438 hivyo matarajio ya Serikali ni kwamba watumishi 438 wenye sifa ya kupatiwa nyumba waliopo Dar-es- salaam watapata makazi hapa Dodoma.

Amesema kuwa nyumba ambazo zinakabidhiwa kwa Wakala wa Majengo ni nyumba za kuishi ambazo awali zilimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu na kuhamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na kutokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli nyumba hizo kwa sasa zitakuwa zikimilikiwa na Wakala wa Majengo (TBA) ili nyumba hizo zitumike kwa watumishi wa Serikali wanaohamia Dodoma.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Serikali ya kukabidhi nyumba za makazi kwa Wakala wa Majengo Tanzania kwa kuwa Dodoma sasa ni Makao Makuu ya Nchi.

Wakati huo Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Majengo Tanzania Msanifu Majengo Elius Mwakalinga amesema kuwa kumekuwepo na tatizo kubwa la upatikanaji wa nyumba kwa watumishi wa umma hivyo nyumba 438 zitasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa nyumba hasa kwa watumishi wanaohamia Dodoma.

Amesema kuwa kwa Mkoa wa Dodoma Wakala wa majengo,Tanzania (TBA) ilikuwa na nyumba zaidi ya 400 ambazo zilikuwa kwenye maeneo ya Area D na Kisasa hivyo kwa nyumba hizo sasa watakuwa na jumla ya nyumba zaidi ya 800.

CANEDUCATE YATOA VITABU KWA WANAFUNZI

Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia umetoa msaada wa vitabu vya ziada 285 kwa wanafunzi 200 wa Shule ya Sekondari Bugisha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za mgodi huo kusaidia maendeleo ya elimu nchini.

Msaada huo ni sehemu ya ufadhili ndani ya programu ya CanEducate inayoendeshwa na kampuni hiyo.

CanEducate ilianzishwa mwaka 2010 lengo kuu likiwa ni kudhamini wanafunzi wa shule za sekondari kutoka katika familia maskini.

Chini ya programu hiyo, wafanyakazi huchangisha fedha chini ya mfuko maalumu na kisha kampuni ya Acacia hutoa kiwango sawa na kile kilichochangishwa.

Fedha hutumika kulipa ada za shule, kununua sare, vitabu na vifaa vya shule kwa wanafunzi.

Wakati wa kuanzishwa kwake, mpango huo uliwasaidia wanafunzi 158 walio karibu na Mgodi wa Dhahabu ya Bulyanhulu.

Hata hivyo, kutokana muitikio mkubwa kutoka kwa wafanyakazi na makandarasi wa Acacia, programu imeweza kukua zaidi na kuwafikia zaidi ya wanafunzi 800 kutoka shule zinazoizunguka Buzwagi.

Moja ya sababu ambazo zinachangia kufanya vibaya kwa wanafunzi katika mitihani yao ya kidato cha nne na cha sita, ni ukosefu wa vitabu mashuleni, na gharama za vitabu ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa kifedha wa wazazi na walezi.

Katika eneo la Buzwagi, mpango huo unahusisha shule tatu za sekondari; Shule ya Sekondari ya Bugisha, Shule ya Sekondari ya Mwendakulima, na Shule ya Sekondari ya Nyasubi ambazo zimetoa wanafunzi bora katika mitihani ya kidato cha nne na kidato cha sita.

Msaada uliotolewa kwa Shule ya Sekondari ya Bugisha ulisimamiwa na maafisa mahusiano ya jamii wa mgodi wa Buzwagi, Yunia Wangoya na Antonia Kiondo.

Msaada huo ulitolewa mbele ya walimu, wazazi na wanafunzi ambao kwa pamoja walitoa shukrani zao za dhati kwa kampuni ya Acacia kwa kuwezesha upatikanaji wa msaada huo mkubwa.

WATUMISHI NA MZABUNI WALAMBA MAHABUSU

Serikali ya Mkoa wa Tabora imeagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Mzabuni Muhoro Traders kwa tuhuma za udanganyifu wa ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 23.2.

Agizo hilo limetolewa leo mjini Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Amesema kuwa kwa nyakati tofauti za kuanzia Januari na Machi mwaka huu watumishi walikula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu jumla ya shilingi milioni 23,202.500.00 mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

Mwanri anaongeza kuwa watumishi hao waliagiza vifaa hivyo kutoka kwa Mzabuni Muhoro Traders wa Igunga vifaa , lakini havikuwahi kupokelewa na Halmashauri ya Igunga lakini kwenye vitabu vya Afisa Ugavi na yule wa Bohari walikiri kupokea katika vitabu vyao.

Anasema kuwa katika hati namba ya malipo namba 2071-1457 watuhumiwa walichukua shilingi 9,250,000/-, hati namba 2017-1457 walijipatia shilingi 6,850,000/- na hati ya malipo namba 2017-1453 shilingi 7,102,500/- na kusababishia Halmashauri hasara hiyo.

Mwanri amewataja walikamatwa ni pamoja na aliyewahi kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga Godfrey Mgongo, Afisa Ugavi Mohamed Mtao, aliyekuwa Mhasibu wa Idara ya Afya sasa yuko TARURA Richard Byelembo na Boharia wa Idara ya Afya Jones Lotto.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza pia Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga wa sasa Dkt. Bonaventura Kalumbete ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri amewaagiza kushughulikia tatizo la ukosefu wa dawa katika Zahanati kwa sababu tayari Halmashauri hiyo imepokea miliomi 550 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

BEI DIRA YA MSIMU WA 2017/2018 HII HAPA

Bodi ya Korosho Tanzania, kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 5 (3)(d) imetangaza bei elekezi kwa msimu 2017/2018.

Akitangaza bei hiyo hapo jana mbele ya vyombo vya habari Jijini Tanga, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Mamam Anna Abdalah, amesema kuwa bei ya kilo moja ya Korosho ghafi daraja la kwanza (Standard Grade ) itakuwa shillingi 1,450/= na kwa Korosho ghafi daraja la pili (Under Grade ) itakuwa shillingi 1,160/=

Mama anna Abdalah ameeleza kuwa bei hiyo imefikiwa baada ya kufanya utafiti wa kupata gharama halisi za kuzalisha kilo moja ya korosho ghafi,na kuongeza asilimia 20 kwa faida ya mkulima.

Pamoja na bei hiyo elekezi, pia Bodi ya korosho imetangaza kuwa msimu wa ununuzi wa korosho 2017/2018 utafunguliwa rasmi tarehe 1/10/2017.

Taarifa hiyo imewahimiza wadau wote wanaohusika na uuzaji na ununuzi wa zao la korosho kukamilisha maandalizi ya msimu kabla ya ununuzi kuanza, ili kuepuka usumbufu.

Ufunguzi rasmi wa soko la korosho msimu wa 2017/2018, ​​umefanika ikiwa ni siku moja baada ya kufanyika kwa kikao cha wadau na watendaji mahususi wa zao la korosho, ambo ulifunguliwa rasmi na waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Kssim majaliwa.

TAKUKURU YATOA NENO KWA WANANCHI WA MTWARA

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoani Mtwara imewataka wananchi mkoani hapa kutoa ushirikiano ili waweze kufikia malengo ya kudhibiti rushwa.

Wito huo umetolewa mapema hii leo na kamanda wa Takukuru mkoa wa Mtwara Domina Mukama, wakati akizungumza na Safari Media, ambapo amesema kuwa kesi ambazo zipo mahakamani hadi sasa zipo 21,huku Manispaa ya Mtwara Mikindani 2, wilaya ya Newala 5,Tandahimba 3,Masasi 8 na Nanyumbu 3.

Aidha Mukama amesema kesi ambazo zimepata suluhisho katika kipindi cha Julai 2016 hadi Juni 2017, kesi 22 zilitolewa maamuzi mahakamani.

Kamanda huyo amebainisha Changamoto wanazokutana nazo ni pamoja kukosa ushirikiano na mashahidi wa kesi husika na kingine kwenda tofauti na maelezo yao ya awali pamoja na kutofika kabisa mahakamani jambo ambalo linadhoofisha juhudi za kupambana na rushwa.

Hata hivyo mafanikio ambayo wameyapata kutoka kwa wananchi ni ushirikiano wa kutoa taarifa kwa kipindi cha julai 2015 hadi juni 2016 walipokea malalamiko 279 na kuanzia juni 2016 hadi juni 2017 walipokea malalamiko 239.

Amebainisha kuwa elimu kwa Umma kuhusu ubaya wa Rushwa kwa wananchi imekuwa ikitolewa mara kwa mara ili kujua haki yake na kupinga rushwa nchini

MAJALIWA AGEUKA MBOGO JUU YA ULANGUZI KATIKA ZAO LA KOROSHO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Viongozi wa Serikali wasiokuwa na mashamba ya mikorosho kutojihusisha na biashara ya uuzaji wa zao hilo.

Waziri Mkuu ametoa agizo,jana Septemba 17 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika mkoani Tanga.

Amesema kama viongozi hao wanahitaji kuuza korosho watumie muda huu ambao Serikali inahamasisha watu wafungue mashamba mapya nao watumie fursa hiyo na kulima.

Amesema ni vema kila mdau akahahakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo kama ni mkulima alime kwa kuzingatia stadi za kilimo na mnunuzi azingatie taratibu zilizopo.

Waziri Mkuu amesema Bodi ya Korosho inatakiwa kuhakikisha inaimarisha zao hilo na kuishauri vizuri Serikali kuhusu namna bora ya kuliendeleza.

Amesema Serikali inaamini kuwa iwapo kila mdau wa zao la korosho atatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuliendeleza zao hilo kila upande utanufaika kikamilifu.

SERIKALI YALIFUNGIA GAZETI LA MWANAHALISI KWA MIAKA MIWILI

Serikali imesitisha uchapaji na usambazaji wa gazeti la Kila wiki la MWANAHALISI kwa kipindi cha miezi ishirini na nne (24) kuanzia leo Septemba 19,2017, kufuatia mfululizo wa gazeti hilo kukiuka maadili, misingi na sheria za taaluma ya uandishi wa habari, kuandika habari zinazo daiwa kuwa za uongo, uchochezi na kuhatarisha usalama wa Taifa.

Zuio hilo pia linahusu toleo la mtandaoni la gazeti hilo.

JET YAIOMBA SERIKALI KUFUNGUA MAKUCHA MGOGORO WA ARDHI KILWA

Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET) kimeitaka serikali kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliopo baina ya wanavijiji wa Mavuji, Migeregere, Liwiti na Nainokwe wilayani Kilwa na Kampuni ya Uwekezaji ya Bioshape Ltd ,uliobuka baada ya kampuni hiyo kuitelekeza ardhi ya vijiji hivyo kwa muda mrefu.

Akizungumza na wanahabari mapema jana Septemba 17, 2017 jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Bodi ya JET, Leah Mushi amesema muwekezaji huyo amekiuka makubaliano ya umiliki wa ardhi takribani hekta 64,000 ikiwemo kwa kutotimiza malengo ya mradi sambamba na kutotekeleza ahadi aliyoahidi ya kuboresha huduma za jamii kwenye vijiji husika.

Kufuatia ukiukwaji huo uliofanywa na kampuni hiyo, Mushi ameitaka serikali kuchukua hatua kwa kuwarudishia wanavijiji hao ardhi yao ili wajikwamue kiuchumi, kama ilivyofanya kwa wawekezaji wengine wasioendeleza ardhi zao

“Kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi, serikali haina budi kuwarudishia ardhi hiyo ili serikali za vijiji ziweze kumiliki misitu na rasilimali nyingine zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi bila kutegemea ruzuku kutoka halmashauri ya wilaya,” amesema.

Kwa upande wake Aisia Rweyemamu miongoni mwa waandishi wa habari za mazingira aliyefanya utafiti wa uwekezaji wa kilimo cha mibono, amesema kufuatia uchunguzi walioufanya hasa kwenye vijiji hivyo vinne walibaini kuwa uwekezaji huo uliathiri wananchi baada ya muwekezaji huyo kusitisha miradi huku akihodhi ardhi kubwa ambayo wananchi hawawezi kuitumia.

Hata hivyo, Rweyemamu amesema Kampuni ya Bioshape Ltd baada ya kushindwa kuendeleza ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka mitano, walitaka kuhamisha uwekezaji huo kwa kampuni nyingine ya uwekezaji kitendo kilichopingwa na wananchi wa vijiji hivyo.

Naye Mosses Masenga alibainisha kuwa, kufuatia uchunguzi walioufanya kwenye vijiji hivyo waligundua kwamba muwekezaji alivyochukua eneo hilo alifoji hati ya tathimini ya athari za kimazingira, pamoja na kumilikishwa eneo hilo kinyume na sheria ikiwemo kuongezewa muda wa kumiliki ardhi hiyo kutoka miaka 33 hadi zaidi ya 90.

Page 10 of 168