blog category

NKAMIA ATAKA VIONGOZI KUKAA MADARAKANI MIAKA SABA

Mbunge wa jimbo la Chemba, Juma Nkamia (CCM) amethibitisha kuwa leo anapeleka hoja binafsi kwa spika wa bunge kuhusu uchaguzi mkuu nchini ufanyike kila baada ya miaka saba na isiwe mitano kama sasa ili kuepuka gharama kubwa ambazo huwa zinatumika.

Mh. Nkamia amesema kuwa yeye ameamua kupeleka muswada huo binafsi kwa spika wa bunge kutokana na serikali kutumia gharama kubwa za kufanya uchaguzi kwa wakati mmoja yaani ule wa serikali za mitaa pamoja na ule mkuu.

"Napeleka hoja au muswada binafsi kwa Spika wa bunge tulijadili hili kama linaweza kufanywa sheria lifanyike.

Ndani ya bunge kuna viongozi wetu wa chama kwa hiyo lazima nipeleke kwao ili kujadili na wao waweze kupitisha kama watakubaliana na mimi na kama ikifanikiwa kufika kwa rais basi iwe sheria ambayo itatuoongoza," amesema Nkamia.

"Nikipeleka hoja yangu kwa Spika nitachanganua gharama zinazotumika kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja uchaguzi mkuu.

Tunaweza kufanya uchaguzi wote kwa pamoja kama wenzetu mfano Kenya wanakuwa na maboksi mengi sana wakati wa kura, hata sisi tunaweza kufanya kama wenzetu badala ya kutumia gharama mbili kwa kipindi kimoja" aliongeza Nkamia.

Aidha, Mh. Nkamia amefafanua kuwa aeleweke kuwa hajamlenga rais aliyoko madarakani ndiye aanze kwenda miaka saba bali ni kwa viongozi wote na kama wazo lake likitimia wakati Rais Magufuli akiwa madarakani nayo si vibaya.

Pamoja na hayo Mh. Nkamia amesema kuwa watu wengi na waoga wa kutoa hoja zao kwa kufikiria wananchi watamfikiriaje hivyo kwa upande wake huwa hana woga wowote linapokuja suala la kusimamia hoja.

DC KILOLO AWAGEUKIA WAZAZI, ATAKA KUWASOMESHA WATOTO WAO

Wanachi wa kijiji cha mwatasi wamekuwa kikwazo cha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo ya shule ya msingi kutokana na wazazi kutowatimizia mahitaji muhimu watoto wao pindi waendepo shule.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika shule hiyo mwalimu mkuu wa shule ya msingi mwatasi Seth Mfikwa alisema kuwa wazazi wengi wa kijiji hicho wamekuwa kikwazo cha maendeleo ya wanafunzi kwa kuwakatisha tamaa juu ya umuhimu wa elimu.

Mfikwa alimuomba mkuu wa wilaya ya kilolo Asia Abdallah kutafuta wataalam wa saikolojia kuja kuwapa elimu wazazi wa kijiji cha Mwatasi ili kukuza taaluma kwa wanafunzi wa kijiji hicho.

Aidha Mfikwa alisema kuwa wamekuwa wakiitisha mikutano ya mara kwa mara lakini bado tatizo kubwa hivyo jitihada zinahitajika kukomesha tabia hiyo kwa kuwa bila hivyo watoto wa kijiji hichi wataendelea kuwa wafanyakazi za ndani tu.

Anderson Mdeke ni diwani wa kata ya Bomalang’ombe alikiri kuwa wazazi wa kijiji cha mwatasi hawana elimu juu ya umuhimu wa kujua dhamani ya elimu katika maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.

Mdeke alisema kuwa uongozi wa kata ya bomalang’ombe utaendelea kutoa elimu kwa wazazi hao ili kurudisha morali ya kuendelea kuwapa mahitaji muhimu yanayohitajika shuleni kwa kwa lengo la kuboresha maisha ya watoto hao.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah aliahidi kulifanyia kazi tatizo hilo kwa kuzungumza na wazazi ili kuwaelimisha juu ya umuhimu wa elimu kwa wananchi wa kijiji hiki cha Mwatasi.

Aidha mkuu wa wilaya hiyo Asia alisema anatakiwa kujifunza tabia za wananchi wa kijiji cha Mwatasi kwanini wanafanya hivyo kwa kuwa changamoto hiyo ni kubwa na inatakiwa kutatuliwa mapema.

Abdallah alisema licha ya changamoto hiyo ya wazazi hata walimu wa shule wanamatatizo kwani haiwezekani kuwa na walimu wengi hivi lakini ufaulu bado upo chini lazima kukaa chini na hawa walimu kujua tatizo ni nini.

RC MBEYA ATOA MIEZI MITATU KWA HALMASHAURI KUJI TATHMINI

Halmashauri ya Mbeya imepewa miezi mitatu kubadili mwenendo wake wa kutoa maamuzi yasiyofuata kanuni, taratibu na sheria, kwa maelezo kuwa yamekuwa yakiingizia serikali hasara ya mamilioni ya shilingi ambapo mkuu wa mkoa Amos Makala pia ameonya kuwa ikiwa itashindwa kujirekebisha atashauri mamlaka husika kuichukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuivunja.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Gabriel Makala amefikia hatua hiyo baada ya uongozi wa halmashauri ya Mbeya , kudaiwa kukaidi ushauri inaopewa na viongozi wa serikali na kutoa uamuzi mbovu, ikiwemo kuwafukuza kazi watumishi wanne bila kufuata taratibu, hivyo kupelekea watumishi hao kukata rufaa kwenye tume ya utumishi wa umma, na kushinda rufaa hiyo, ambapo tume imeamuru warejeshwe kazini na walipwe stahiki zao.

Aidha Mkuu wa mkoa pia amewaonya baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo, a kujihusisha na siasa kutoa taarifa za upotoshaji kwa madiwani ambazo ndizo zinasababisha kutolewa kwa uamuzi ambayo si sahihi.

Mwalingo Kisemba ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya anasema halmashauri yake ilitimiza wajibu wake na kwamba kushinda rufani ni sehemu ya utaratibu na ni haki ya mtumishi na kwamba halmashauri yake haina tatizo na uamuzi huo.

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Agosti mwaka huu alifanya ziara Mkoani Mbeya na kuitadharisha halmashauri ya wila ya Mbeya kuwa uamuzi wake wa kuwafukuza watumishi bila kufuata taratibu inaweza kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya zaidi ya shilingi milioni 400.

MWANRI ACHARUKA TENA ,AMTEUA DC WA TABORA KUONGOZA UKAGUZI WA VIWANDA

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameteua Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi kuongoza Kamati aliyoichagua kwa ajili ya kufuatilia viwanda mbalimbali ili kuangalia hali halisi na kama vimeshindwa kufanyakazi viweze kupewa wawekezaji wengine.

Mwanri aliteua Kamati hiyo jana mjini Tabora wakati wa Mkutano na wadau mbalimbali na Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora.

Wengine waliochaguliwa ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philipo Ntiba ,Afisa Biashara Mkoa Lucas Kusare ambaye ni Katibu wa Kamati, Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Richard Lugomela na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Tiganya Vincent.

Alisema kuwa Kamati hiyo itaanza na Kiwanda cha Nyuzi Tabora ambapo itaangalia mpango kazi wake, itakagua mashine zote kama zinafanyakazi na uwezo wa kifedha wa mwekezaji huyo kama anao mtaji wa kutosha wa kuendesha kiwanda.

Mambo mengine yatakayofuatiliwa na Kamati hiyo ni pamoja na kuangalia matatizo ambayo Mwekezaji huyo aliyaeleza kuwa ukosefu wa soko la nyuzi zake kutokana na viwanda ambavyo ndio vilikuwa vikinunua kwake kuanza kuagiza toka nje bidhaa hizo.

Mkuu huyo Mkoa aliongeza kuwa mambo mengine ambayo Kamati itayafanya ni kuangalia fursa za masoko ya bidhaa za Kiwanda hicho kama vile Bohari Kuu za Dawa(MSD), Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) na wafanyabiashara wengine wanaweza kununua bidhaa zake.

Alisema kuwa Kamati hiyo itatakiwa kila baada ya siku tatu impelekee taarifa ya maendeleo ya kazi yao.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa mwezi mmoja kwa Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora kuhakikisha mashine zake zinafanyakazi.

Alisema kuwa baada ya kipindi kuisha atakwenda kukagua na akikuta hakuna kitu atalazimika kumuomba Waziri wa Viwanda aje kuchukua hatua ikiwemo kumpa mwekezaji mwingine.

Mkuu huyo Mkoa alisema kuwa hata kama mali ghafi kwa sasa hivi hakuna anataka ni kujiridhisha kuwa mashine zote ni zima wakati akiwa anasubiri msimu wa pamba ujao ili apate mali ghafi.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora yuko katika zoezi la kuhakiki viwanda vyote ili kujiridhisha kama vinafanyakazi na vile ambavyo wamiliki wake wameshindwa waweze kuvirudisha Serikalini

RAIS MAGUFULI AVUNJA MAMLAKA KIGAMBONI

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amevunja Mamlaka ya uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) kuanzia leo Septemba 13, 2017.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Hashim Mgandilwa amethibitisha hilo na kusema kuwa Rais Magufuli ni msikivu kwani amesikia kilio cha watu wa Kigamboni na kuamua kuivunja mamlaka hiyo ya Uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA).

"Usikivu ni sehemu ya utatuzi hatimaye Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli aridhia uvunjwaji wa Mamlaka ya uendelezaji wa mji wa Kigamboni (KDA).

Akizungumza Waziri wa Ardhi Mhe. Lukuvi leo katika ukumbi wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere amesema "Mhe. Rais ameniagiza niwaalifu kuwa leo amevunja rasmi KDA, Ahsante Mhe. Rais kwa kutusikiliza" alisema Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mgandilwa

Mwezi Juni, mwaka huu Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile aliiomba serikali kukabidhi majukumu yote, yaliyokuwa yakifanywa na KDA kwa Halmashauri ya Manispaa hiyo ili kuyatekeleza na kuendeleza mji mpya wa Kigamboni.

MSINILETEE ORODHA YA WALIO HUKUMIWA KUNYONGWA- RAIS MAGUFULI

Rais John Pombe Magufuli amefunguka na kutoa kauli yake kuhusu baadhi ya wafungwa ambao wamehukumiwa kunyongwa kutokana na makosa mbalimbali na kudai kuwa yeye anaogopa kusaini ili wafungwa hao wanyongwe.

Rais Magufuli amesema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaama wakati akimuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma na kusema anatambua kuwa idadi wa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa ni wengi sasa ila anaomba asipewe hiyo orodha.

"Sisi wanasiasa tunaogopa kunyonga, natambua kuwa sasa orodha ya watu ambao wanatakiwa kunyongwa ni kubwa sana ila mimi naomba hiyo orodha msiniletee kwa sababu najua ugumu wake ulivyo" alisisitiza Rais Magufuli

Mbali na hilo Rais Magufuli amesema kuwa amechukua muda mrefu kumteua Jaji Mkuu wa Tanzania kutokana na ukweli kwamba alikuwa anatafuta mtu ambaye anaweza kuendana na dhamira yake ya kupambana na rushwa hivyo alipojilidhisha na jaji huyo ndiyo maana ameamua kumteua kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA WAFANYABIASHARA NCHINI

Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuvutia wafanyabiasha wa ndani na nje ya nchi.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo leo mjini Dodoma wakati akizindua awamu ya tano ya programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za Umma 2017/18 na 2021/22.

Akifafanua Mhe. Samia amesema kwamba katika kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi mzuri wa fedha za umma, Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kuwa wafanyabishara wote wanatumia mfumo wa kielekroniki kulipa kodi.

Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kupunguza matumizi ya fedha katika Wizara, Taasisi na Idara zake ili fedha hizo ziweze kutumika katika kuboresha huduma za jamii.

Naye, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha umeleta mafanikio makubwa ambapo umeongeza makusanyo na mapato ya Serikali Tanzania Bara na Visiwani.

Vile vile katika awamu hii maboresho ya kazi za wakaguzi wa ndani katika Wizara, Taasisi, Idara pamoja mamlaka ya Serikali za mitaa nchini.

Maboresho ya programu ya usimamizu wa fedha za Umma ulianza mwaka 1998 ikiwa ni awamu ya kwanza ambayo ilihusisha uthibiti matumizi ya Serikali na kuchangia kukuza uchumi endelevu. Awamu ya pili ilifanyika mwaka 2004 – 2008 ambayo ilijikita katika kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kutumia viwango vya kimataifa.

Awamu ya tatu ilifanyika mwaka 2008 – 2012 ambayo ilihusisha katika kuhakikisha mbinu na mifumo iliyowekwa awamu ya kwanza inaoanishwa na kutumika ipasavyo kuleta matokeo yaliyokusudiwa na awamu ya nne ilikuwa mwaka 2012-2017 ambayo ilenga katika nidhamu katika usimamizi wa fedha za umma na kutoa huduma bora kwa Umma ili kuleta maendeleo endelevu.

MAKUNDI YA WAKIMBIZI RAIA WA BURUNDI KUIONA ARDHI YA KWAO WIKI HII

Makundi mawili kila moja likiwa na wastani wa wakimbizi 350 raia wa Burundi kati ya wakimbizi elfu 13,000 ambao hadi tarehe 07 Septemba, 2017 walikuwa wamejiorodhesha kwa hiari kurejea nyumbani yanatarajiwa kuondoka nchini wiki hii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wakimbizi, katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Deusdedit Masusu, misafara saba yenye wastani wa wakimbizi 350 inatarajiwa kuondoka nchini kurejea Burundi katika mwezi huu wa Septemba, miwili kati ya hiyo ikiondoka siku ya Jumanne tarehe 12 na Alhamisi tarehe 14 Septemba, 2017.

Bwana Masusu amesema kuwa idadi ya wakimbizi wataorejeshwa nyumbani inatarajiwa kuongezeka kadri zoezi hilo ambalo lilianza Alhamisi wiki iliyopita litakavyoshika kasi.

Mkurugenzi Msaidizi huyo alieleza kuwa kasi ya kujiandikisha kwa hiari kwa wakimbizi hao raia wa Burundi inatarajiwa kuongezeka zaidi kufuatia makundi hayo kurejea nyumbani kwa kuwa mafanikio ya zoezi hilo yatakuwa kichocheo kwa wengine kutaka kurejea nyumbani.

Amebanisha kuwa urahisi wa mawasiliano utawezesha wakimnizi waliorejea kuwapa wenzao mrejesho wa hali ilivyo nchini kwao na hivyo kutoa hamasa kwa walioko makambini nao kutaka kurejea nyumbani.

Mkurugenzi Msaidizi huyo aliongeza kuwa kinachofanyika ni kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ili wakimbizi hao waweze kurejea nyumbani kwa usalama na heshima.

Page 9 of 165