blog category

ASKOFU GADI ASIMAMIA IBADA YA KUOMBA MVUA NCHINI

Askofu wa Kanisa la Habari Njema kwa Wote la Jijijni Dar es Salaa, Charles Gadi pamoja na wasaidizi wake, wameendesha maombi maalum ya kuliombea Taifa mvua, ili ziweze kusaidia wananchi na viumbe vyote vinavyotegemea maji kupitia Baraka za mvua sehemu mbalimbali.

Tukio hilo limefanyika mapema leo Septemba 18,2017, Jijini Dar es Salaam, Askofu Gadi aliambatana na wasaidizi wake na kuliombea Taifa mvua huku akiwataka wananchi nao kuungana katika maombi hayo kwani ardhi ikiendelea kuwa kame viumbe vitapoteza maisha na hata kusababisha majanga katika nchi.

“ Hivi karibuni Mamlaka ya hali ya hewa wametoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea upungufu mkubwa wa mvua za vulikwenye mikoa mingi hapa nchini.

Sisi kama viongozi wa dini tunakubaliana na utabiri huo wa Kisayansi na ambao mara nyingi ufanikiwa, lakini haitakuwa sawa kusubiri hadi ukame utokee wakati Mungu ametupa imani na mamlaka ya kuombea dhidi ya majanga kama hayo.

Sisi kama Goods News for All, kwa kushirikiana na dini na madhehebu mbalimbali tumekuwa tukiendesha mikutano ya kuomba dhidi ya ukame tangu mwaka 2006, ambapo ni zaidi ya miaka 11 sasa” alieleza Askofu Gadi.

Askofu Gadi aliongeza kuwa, viongozi wengine wa dini kwa pamoja nao wanayo nafasi ya kuliombea Taifa katika hilo ili ukame usitokee. Ukame ni jambo baya na kwa uchumi, ni baya kwa afya na watu na tena ni baya viumbe hai wote wakiwemo wanyama na mimea.

Aidha, Askofu Gadi alinukuu baadhi ya vifungu vya Biblia ikiwemo: Kumbu kumbu 28:12 “ Atakufunulia bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; Nawe utakopesha mataifamengi,wala hutakopa wewe.

Vifungu vingine ni pamoja na : Mathayo 5:45, Matendo ya Mitume 15:17 na kitabu cha Yakobo 5:17-18.

Katika hitimisho hilo, Askofu Gadi ameweka wazi kuwa, kwa maandiko hayo ya Biblia, yanaonyesha wazi kwaba mvua ni mali ya Mungu, na ameahidi pasipo shaka kwamba tukimuombaanatupatia.

SERIKALI KUWAKABILI VIWAVIJESHI AINA YA ‘FALL ARMYWORM (FAW)’

Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imeanza jitihada za kuwakabili Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wanaojulikana kitaalamu kama Spodoptera Frugiperda ambao wametajwa kuwa na uwezo mkubwa kuharibu mazao mbalimbali hususan mahindi ambayo ndio zao kuu la chakula nchini.

Imeelezwa kuwa Viwavijeshi hao wanapofika kwenye mazao hutoa kemikali ambayo huweza kudanganya mmea kuwa unashambuliwa na magonjwa kama ukungu au fangasi hivyo mmea unapohisi unashambuliwa na hayo magonjwa, hupunguza kinga dhidi ya wadudu hao hatari na kuwa rahisi kushambuliwa.

Hayo yamebainishwa Septemba na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema wakati akifungua warsha ya siku moja mbele ya Wadau wa Kilimo ambao ni Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani USAD, ONE HACKER FUND, Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Mradi wa WEMA .

Mkutano ulikuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kwa ajili ya kumkabili mdudu huyo aina ya Fall Armyworm (FAW) ambaye anashambulia mazao mbalimbali nchini hususani zao la mahindi.

Amesema kuwa Athari ya viwavi jeshi haishii kuharibu majani ya mimea pekee, wadudu hao wanapokula majani na kutengeneza sumu aina ya ‘firenide’ inayodhuru mifugo inapokula majani yaliyoathiriwa.

Bwana Malema amesema tayari Serikali imechukua juhudi za awali kukabiliana na mdudu huyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya utambuzi wa mdudu huyo kwa kuwataka Wananchi kung’oa mazao na kuyachoma pindi wanapobaini uwepo wa mdudu huyo.

Pia tayari dawa tatu zimepitishwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya uchunguzi wa Viatilifu (TPRI) zinazoangamiza wadudu hao ambazo ni Duduba 450, Mupacrone 500 EC na Match Save kutoka Kampuni ya Syngenta hivyo Wananchi wametakiwa kuzitumia haraka pindi wanapoona dalili za kuwepo wa wadudu hao shambani.

Bwana Malema amesema kuwa katika kipindi cha miaka mingi Tanzania imekuwa ikikumbwa na viwavijeshi aina ya African Armywarms ambapo mara zote imekuwa ikiwadhibiti wadudu hao wanapojitokeza kwa kuwapa kiuatilifu kinachosababaisha matumbo ya wadudu hao kujaa na hatimaye kuwasababishia vifo.

Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza Wizara ilipata taarifa ya uvamizi katika shamba la Mwekezaji mkubwa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa mwezi Machi 2017 na walipofuatilia na kupeleka sampuli maabara mdudu huyo alibainika kwa jina la Spodoptera frugiperda au Fall arymworm ambaye ni hatari na amekuwa akiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Kutokana na unyeti wa suala hilo Wizara ya Kilimo imewasiliana na Shirika la Chakula Duniani (FAO), kwa ajili ya kuunganisha juhudi za pamoja ili kumdhibiti mdudu huyo kabla hajasambaa kwenye maeneo mengi nchini.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika taarifa yake imesema viwavijeshi hao aina ya Fall armyworm wameonekama pia katika nchi za Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Namibia Afrika ya Kusini na Zambia huku chanzo chake ikiwa ni nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Redio ya Umoja wa Mataifa, FAO bado haijatangaza kiwango kamili cha uharibifu katika nchi hizo, huku ikiongeza kuwa Shirika hilo na Wadau wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamejadili udhibiti wa viwavijeshi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Mimea, Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bibi Beatrice Palangyo akiwasilisha mada ya utambuzi wa wadudu hao katika warsha hiyo amesema kuwa katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wadudu hawa walianza kuingia nchini Nigeria na kwa sasa wameenea katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Afrika kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Malawi.

Amesema wadudu hao wanashambulia mazao ya jamii ya nafaka kama mahindi (Corn) wanauwezo wa kushambulia hata magugu pale wanapokosa mazao kama mahindi kwani hawali mazao mengine kama mboga na matunda, wanakula zaidi mahindi na magugu yanayofanana na mahindi.

Zaidi ya Mikoa 15 nchini ikiwemo Zanzibar imeripoti kuwepo kwa kadhia ya mdudu huyo hivyo asilimia 15 ya mazao jamii ya nafaka kama mahindi yameathiriwa, jambo ambalo kama lisingepatiwa ufumbuzi wa haraka, lingesababisha upotevu mkubwa wa mazao mashambani na kutishia upatikanaji wa chakula nchini.

WAKAZI WA MTAMBASWALA MTWARA WALAMBA DUME

Wakazi wa mji mdogo wa Mtambaswala uliopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji wilayani Nanyumbu sasa wameondokana na adha ya kutembea umbali wa kilometa sabini kufuata huduma za afya baada ya majengo yaliyokuwa yanatumika na wakandarasi wa daraja la Mtambaswala kuwa kituo cha afya ambacho kimefunguliwa.

Majengo yaliyokuwa yanatumika na wakandarasi waliojenga daraja la Mtambaswala ndiyo yamekuwa kituo cha afya baada ya mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego kuamuru majengo hayo kuwa kituo cha afya ili kuwasaidia wakazi wa mji mdogo wa Mtambaswala waliokuwa wanatembea umbali wa kilometa sabini kufuata huduama za Afya.

Kituo kimefunguliwa rasmi na huduma kadhaa zinatolewa,jambo hili ni la furaha sana kwa wakazi wa mji huo.

Mkoa wa Mtwara unakabiliwa na upungufu wa vituo vya afya ambapo kituo hicho kinafanya mkoa kuwa na idadi ya vituo kumi vya afya kati ya kata 191 za mkoa huo na kwamba serikali ya mkoa inatumia fursa ya majengo ya wakandarasi na kuyafanya kuwa kituo cha afya.

SERIKALI CHEMBA, DODOMA KUZUIA MIFUGO YA WAGENI

Serikali wilayani Chemba mkoa wa Dodoma imewagiza viongozi wa serikali za vijiji, kata na tarafa katika wilaya hiyo kuacha mara moja tabia ya kuwakaribisha wageni kutoka mikoa ya jirani wanaoingia na makundi ya mifugo na kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Simon Odunga wakati akiongea na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini na akaeleza kuwa mifugo inayoingia kwenye wilaya hiyo pia imekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira katika pori la akiba la Swagaswaga.

Bwana Odunga amesema hivi karibuni zaidi ya ng’ombe 250 wamekamatwa wakichunga katika pori la akiba la Swagaswaga kinyume cha sheria za uhifadhi na kwamba serikali itachukua hatua kali dhidi ya wote wanaoingiza mifugo kwenye pori hilo kinyume cha sheria.

Kuhusu wananchi waliowavamia askari wa wanyamapori wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mishale ya sumu wakitaka kupora mifugo iliyokamatwa hifadhini, mkuu wa wilaya amesema kitendo hicho hakikubaliki na amewaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani askari hao wako kwa mujibu wa sheria na wanatimiza wajibu wao.

Amesema pori hilo lina rasilimali muhimu ikiwemo wanyamapori adimu na misitu ya vyanzo vya maji kwahiyo lazima lihifadhiwe kwaajili ya matumzi ya vizazi vya sasa na vijavyo na kwamba tayari kuna operesheni inayoendelea kukabiliana na uhalifu unaofanywa na baadhi ya wananchi kwenye pori hilo.

Aidha Bwana Odunga amekitaka chama cha wafugaji kusaidia kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kufuga kisasa na kuvuna mifugo yao waiuze na kujiendeleza kimaisha kwani jamii nyingi za wafugaji zinaishi maisha duni licha ya mifugo mingi waliyo nayo.

Amesema wilaya imeanza zoezi la upigaji chapa wa mifugo kama njia muhimu ya utambuzi wa mifugo iliyoko katika wilaya hiyo zoezi linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa kumi ambapo zaidi ya ng’ombe laki wanatarajiwa kuwekewa alama za utambuzi.

Kwa upande wake Meneja wa pori la akiba la Sawagaswaga Alex Choyachoya amesema kuanzia sasa uongozi wa pori hilo umejipanga kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwemo uingizaji wa mifugo na ujangili wa aina mbalimbali.

Aidha Bwana Choyachoya ameishukuru serikali kwa ushirikiano katika kushirikiana na askari wa mamlaka ya wanyamapori katika pori la akiba la Swagaswaga kwa kuimaimarisha doria zinazlenga kuimarisha vitendo vya uhalifu katika pori hilo.

Kuhusu wananchi waliowavamia askari wa wanyamapori wakiwa na sialaha za jadi ikiwemo mishale yenye sumu wakitaka kupora mifugo iliyokamatwa katika pori hilo alisema watu hao walikamatwa na wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya uhalifu wa kuingia ndani ya pori kinume cha sheria.

NEEMA YANUKIA KWA WAKAZI WA LILUNGU MTWARA

Mwezi mmoja mara baada ya Safari Media kuripoti Adha inayo wakabili wakazi wa kata ya Likonde kutokana na ukosefu wa maji safi, mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mtwara

MTUWASA, imesikia kilio hicho na wameanza kuwafikishia bomba kubwa la kusambaza maji katika mtaa huo.

Wakizungumza na Safari Media kwa nyakati tofauti wakazi wa mtaa huo wametoa shukrani za dhati kwa Safari Redio mara baada ya kupaza sauti zao na mamla hiyo kusikia na kufanyia kazi.

Miungoni mwa wakazi hao ni Bi.Salma Liviga ambae ametoa shukrani zake za dhati kwa Safari Radio na MTUWASA kwa kusikia kilio cha Muda Mrefu na kusema kuwa walikuwa wanateseka sana ili kupata maji lakini kwa juhudi wanazo ziona matumaini makubwa wanayo.

Bi Amina Abdalah ambaye pia ni mkazi wa mtaa wa lilungu ameishukuru MTUWASA na kusema kuwa wanategemea bomba hilo litakuwa msaada kwao kwa kuwapatia maji hayo kwa uhakika bila usumbufu wowote.

Kwa upande wake Mkurugezi mtendaji mamlaka ya maji MTUWASA mhandisi Mashaka Sitta amesema kuwa mamlaka hiyo ilisikia kilio hicho na baada ya kuwafikishia mabomba wananchi wanatakiwa kweda kuchukua fomu ambazo ni bure ili wataalamu waende katika maeneo yao na kuchukua vipimo kwaajili ya kuwaandalia vifaa ambavyo ni gharama ndogo wananchi wanatakiwa wavilipie MTUWASA na baada ya siku saba toka kujiandikisha watapata maji.

Hata hivyo Bwana Sitta amewaomba wananchi wa mitaa hiyo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuchukua fomu kwa ajili ya kuingiziwa maji majumbani mwao.

SERIKALI YAPATA UFADHILI WA BIL. 66

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepata ufadhili wa Shilingi Bilioni 66 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha vituo vya Afya nchini.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Hamisi Kigwangala amesema hayo leo Mjini Dodoma allipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mhe. Khadija Nassir Ali juu ya utekelezaji wa agizo la Mwandoya la kuanzisha huduma za upasuaji katika vituo vyote vya Afya nchini. .

Aidha amesema kuwa, fedha za utekelezaji wamaboresho ya vituo hivyo zimeanza kupelekwa katika halmashauri husika ili kuanza maboresho katika vituo hivyo.

Ameendelea kwa kusema kuwa baada ya muda huo kumalizika, Wizara iliongeza miezi mitatu ili kukamilisha agizo hilo. Aidha wataalam wa Wizara hiyo kwa sasa wanatembelea vituo katika Halmashauri nchi nzima kwa ajili ya kufanya tathmini, kubaini waliotekeleza na ambao hawajatekeleza ili hatua za kinidhamu zifuate.

Wizara hiyo hadi sasa imesambaza vifungashio (delivery packs) 60,000 kwa mikoa sita (6) ya Kanda ya Ziwa ambayo vifo vingi vya mama wajawazito na watoto vimekuwa vikitokea huko. Aidha ni jukumu la kila Halmashauri kuweka mahitaji ya vifungashio kwenye mpango kabambe wa Afya wa halmashauri (Comprehensive Council Health Plan) (CCHP).

DK. MABODI AKEMEA USALITI NDANI YA CCM ZANZIBAR

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi amesema chama hicho hakitowavumilia baadhi ya wanachama na viongozi wanaotumiwa na vyama vya upinzani kuvuruga mshikamano uliopo ndani ya taasisi hiyo.

Ametoa msimamo huo wakati akihitimisha ziara zake za kuimarisha chama na kuwapa mikakati ya kiutendaji viongozi wapya waliochaguliwa katika uchaguzi wa chama hicho kuanzia ngazi za matawi hadi majimbo Unguja, uko katika Tawi la Ijitimai jimbo la Mwanakwerekwe.

Amesema kupitia uchaguzi wa chama unaofanyika kwa ngazi mbali mbali ni lazima wanachama wasaliti wawekwe kando kwa kutopewa nafasi za uongozi na kiutendaji ili kunusuru uhai wa chama hicho kisiasa.

Amewasihi viongozi waliochaguliwa kuzitendea haki nafasi zao kwa kushuka ngazi za chini kutafuta wanachama wapya hasa wa vyama vya upinzani wajiunge na CCM ili mwaka 2020 upatikane ushindi wa kihistoria.

Aidha amewataka viongozi hao wapya kutumia rasilimali watu za wanasiasa wakongwe na wazee wa chama hicho kujifunza itikadi na historia ya chama ili watekeleze kazi zao kwa ufanisi.

Dk. Mabodi alisema chama hicho kina imani kubwa na viongozi wake wa jumuiya na chama waliochaguliwa kuwa watakivusha na kuendeleza mambo mema yaliyoachwa na watangulizi wao.

Amesema CCM inaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 ili kero mbali mbali zinazowakabili wananchi ziweze kutafutiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kupitia ziara hiyo amewaagiza makatibu wa Matawi wa chama hicho pamoja na kamati zingine kuhakikisha wanashuka ngazi za chini za zoni kutafuta wanachama wapya pamoja na kufanya shughuli za kijamii za kuwasaidia wazee katika maeneo mbali mbali nchini.

Sambamba na hayo ametoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi na wanachama wanaouza kadi za uanachama kwa wapinzani na kuwataka waache tabia hiyo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kimaadili kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Naye Katibu wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe , Ramadhan Fatawi amesema Madiwani kwa kushirikiana na Mwakilishi wa jimbo hilo wamesimamia na kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo kusimamia ujenzi wa barabara ya lami inayotoka katika mtaa wa Kwamabata kwenda magogoni iliyogharamiwa na Wizara ya nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara Maalum.

Mradi mingine ni uendelezaji wa ujenzi wa chuo cha Amali cha jimbo hilo, kulipia ada za masomo wanafunzi wa vyuo vikuu na sekondari, kujenga vyoo katika skuli ya Urafiki ya Mwanakwerekwe.

Azitaja changomoto zinazowakabili katika jimbo hilo kuwa pamoja na mafuriko yanayotokea kila mwaka, upungufu wa ajira kwa vijana pamoja idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika darasa moja maskulini.

Pamoja na hayo Katibu huyo ameahidi kuwa Chama cha Mapinduzi ndani ya jimbo hilo kimejipanga kuhakikisha Uchaguzi ujao wanarudisha nafasi ya kiti cha Ubunge kilichoshikiliwa na chama cha upinzani.

SIKU YA KIMATAIFA YA KUPATA TAARIFA KUFANYIKA SEPTEMBA 28

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kupata taarifa inatarajia kufanyika Septemba 28, mwaka huu ambapo wadau wa habari wameiomba Serikali kutekeleza sheria ya kupata taarifa.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Mwenyekiti wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa, Kajubi Mukajanga amesema Serikali na wadau wanao wajibu wa kutekeleza sheria hiyo ilikutoa fursa na haki ya kupata taarifa.

Page 8 of 165