blog category

UBALOZI WA SWEDEN WATOA DOLA MILIONI 36 KWA UN TANZANIA

Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania umesaini makubaliano na Umoja wa Mataifa Tanzania ambapo Sweden imetatoa jumla ya Dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) kwa shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo.

Makubaliano hayo yametiwa saini rasmi na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Katarina Rangnitt na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez, katika ofisi za Ubalozi wa Sweden jijini Dar es Salaam.

Mchango wa Sweden utasaidia jitihada za Umoja wa Mataifa za kuhamasisha ukuaji wa kiuchumi ulio jumuishi na ajira na kuimarisha utawala wa kidemokrasi, haki za binadamu na usawa wa jinsia. Mchango huo pia utasaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na kuondoa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Akifafanua utayari wa dhati wa Sweden katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania, Balozi Rangnitt alieleza kwamba Sweden imechagua kusaidia shughuli za Umoja wa Mataifa zinazoakisi malengo ya maendeleo ya nchi katika nyanja za haki za wanawake, utawala wa demokrasia na ukuaji wa uchumi.

Shughuli hizo ni zile zinazomnufaisha kila mmoja katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa kipato cha kati. “Kwa kupitisha sehemu ya msaada wetu kupitia Mfuko wa Umoja wa Mataifa chini ya Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja, tunashiriki kikamilifu katika kusaidia ufikiwaji wa malengo ya maendeleo ya Tanzania. Vilevile, tunatambua bayana kabisa na kuthamini wajibu uliokubaliwa kuwa ndio wa Umoja wa Mataifa katika kuleta maendeleo endelevu.

Kwa msaada huu, tunawezesha uchukuaji hatua unaoendana na sera ya nje inayozingatia haki za wanawake ya Sweden na pia jitihada zinazolenga, miongoni mwa mambo mengine, ajira yenye hadhi na haki za watoto. Hii inadhihirisha mwendelezo wa uhusiano wa karibu na Umoja wa Mataifa na serikali ya Tanzania wenye lengo la kuleta maendeleo yenye usawa na jumuishi zaidi,” alisema Balozi.

Akisisitiza utayari wa kuendelea kuisaidia Tanzania na Umoja wa Mataifa, Balozi alitumia fursa hiyo kuthibitisha kuyapokea kwa moyo mmoja mageuzi ya Mfumo wa UN chini ya Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja na kutambua njia fungamanifu zinazotumika na thamani inayopatikana kutokana na mchango wa mashirika ya UN katika lengo moja kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, washirika wa kijamii na vyama vya kiraia.

Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Rodriguez alitoa shukrani kwa serikali na watu wa Uswidi kwa msaada wao endelevu akiipongeza Uswidi kwa kuwa mshirika wa maendeleo asiyeyumba katika shughuli za Umoja wa Mataifa Moja na pia kwa Tanzania.

WAHAMIAJI HARAMU 74 WANASWA MTWARA

Idara ya uhamiaji mkoani Mtwara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani humo wamewakamata wahamiaji haramu sabini na wanne (74) raia wa Ethiopia ambao wameingia nchini kinyume cha sheria na kujaribu kuvuka mpaka bila kufuata taratibu za kisheria.

Baada ya kushindwa kuendelea na safari yao ya kuelekea nchini Afrika ya Kusini raia hawa sabini na nne wanajikuta mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama vya hapa mkoani Mtwara,sasa wanalia kilio hawajui cha kufanya.

Idara ya uhamiaji inasema kuwa imewakamata raia hao ambao sitini na saba kati yao wamesafiri kwa usafiri wa boti baharini kutoka Mombasa Kenya hadi katika kisiwa cha Membelwa Msanga mkuu na wengine saba wamekamatiwa wilaya ya Tandahimba hapa mkoani Mtwara.

Wahamiji hao walikuwa na mwenyeji wao kutokea tanga ambae ni mkazi wa kisiwa cha Pemba Bakari Ali Saidi ambae alipewa shilingi laki saba kuwasafirisha wahamiaji hao lakini sasa yupo chioni ya ulinzi.

NECTA YATOA ONYO MITIHANI YA KIDATO CHA NNE

Wanafunzi wa kidato cha nne leo wameanza kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne nchini, hali iliyopelekea Baraza la Mtihani nchini (NECTA) kutoa angalizo la kuwa halitosita kumchukulia hatua mwanafunzi yeyote pamoja wasimizi wa Mitihani hiyo ambao watajihusisha na udanganyifu.

Pia,Baraza hilo limewapa onyo wamiliki wa shule kuacha kuwaingilia wasimamizi wa mitihani hiyo kwakuwa shule zao ni vituo maalum vya kufanyia mtihani.

Onyo hilo limetolewa Jijini Dar es Salaam,na Katibu Mtendaji wa (NECTA), Dkt Charles Msonde wakati wa mkutano na waandishi,amesema Baraza hilo linatoa wito kwa kwa wasimamizi wa mitihani wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu.

“Tunawaasa wasimamizi wa mitihani pamoja na wanafunzi kujiepesha na vitendo vya udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya Taifa” amesema Dkt Msonde.

Amesema Baraza hilo linawataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani na hivyo havitakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi.

“Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha Mitihani endapo litajiridhisha kuwa uwepo wake wa unahatarisha Usalama wa Mitihani ya Taifa” amesema Dkt Msonde.

Hata hivyo, Dkt Msonde amesema Baraza hilo linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri wanafunzi hao kwa kipindi cha miaka mine ya elimu ya sekondari hivyo hakutakuwepo na vitendo vya udanganyifu.

Pamoja na hayo, amesema katika mitihani huo jumla ya watahiniwa 585,938 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 323,513 na watahiniwa wa kujitegemea ni 62,425.

“Kati ya watahiniwa wa shule 323,513 waliosajiliwa ,wanaume ni 159.103 sawa na asilimia 49.18 na wanawake ni 164,410 sawa na asilimia 50.82,huku watahiniwa wenye uono hafifu ni 305 ambapo maandishi yao yanakuzwa”amesema Dkt Msonde.

Kuhusu watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa ni 62,425 ,wanaume ni 28,574 sawa na asilimia 45.77 na wanawake ni 33,851 sawa na asilimia 54.23 huku watahiniwa 6 wasioona. Aidha, Baraza hilo linatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano katika kuhakikisha mitihani hiyo ambayo inaanza kesho Oktoba 30 hadi 17 Novemba 2017 inafanyika kwa Amani na Utulivu huku akiwaomba wananchi hao kuheshimu eneo la mtihani linapofanyika.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII DK.KIGWANGALLA ATEMBELEA NGORONGORO

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amefanya ziara maalum kukagua masuala mbalimbali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro sambamba na kuzungumza na viongozi wa Mamlaka hiyo kwenye eneo la makao makuu yake yaliyopo ndani ya hifadhi.

Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Kigwangalla ameweza kupokea kupokea maoni na masuala mengine ya kuendeleza Mamlaka hiyo ya Ngorongoro.

Waziri yupo Ngorongoro kwa muda wa siku mbili ambapo pia amepata kutembelea maeneo ya hifadhi yenye migogoro na wafugaji.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AFANYA ZIARA DODOMA

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amefanya ziara katika Kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo eneo la Zuzu mjini Dodoma.

Akiwa amefuatana na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu, Naibu Waziri Mgalu, ametembelea Kituo hicho ili kujionea utendaji kazi wake.

Akitoa malelezo kwa Naibu Waziri, Kaimu Mkuu wa Kituo hicho, Bosco Mgina amesema kuwa, Kituo hupokea msongo wa umeme wa kilivolti 220 katika njia tatu ambazo ni Mtera, Iringa One na Iringa Two.

Aidha, ameongeza kuwa, Kituo kina transfoma mbili za kupoza umeme ambapo kila moja ina uwezo wa kutoa megawati 24 za umeme hivyo kufanya jumla yake kuwa megawati 48.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme kwa Mkoa wa Dodoma, Meneja Temu ameeleza kuwa kwa sasa huduma ya nishati hiyo muhimu imerejea katika maeneo yote baada ya jitihada za Shirika hilo katika kutatua matatizo yaliyojitokeza hivi karibuni.

Akihitimisha ziara yake katika Kituo hicho, Naibu Waziri Mgalu amewasisitiza viongozi wa TANESCO kuhakikisha huduma ya umeme wa uhakika inaendelea kutolewa kwa wateja katika maeneo yote.

WALENGWA WA TASAF TABORA WAPOKEA BILIONI 20

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umetumia bilioni 20 ambazo zimetolewa kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Halmashauri zote za Tabora kwa ajili kunusuru kaya maskini katika eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa mjini Tabora na Mratibu wa TASAF Mkoa huo Ngoko Buka wakati wa kikao cha kutathmini utekelezaji wa TASAF Awamu ya Tatu sehemu ya kwanza kilichowashirikisha Wafadhili ,viongozi kutoka makao Makuu TASAF na wale wa Mkoa na Wilaya ya Uyui.

Amesema kuwa fedha hizo zilitolewa katika kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Agosti mwaka huu ambapo jumla ya walengwa 45,928 waliwezwa kunufaika na fedha hizo na hatimaye kubadilisha maisha yao.

Buka amesema kuwa fedha zimesaidia baadhi ya walengwa kuanzisha miradi mbalimbali kama ufugaji wa kuku,bata,mbuzi ,ng’ombe ,ujenzi wa nyumba bora, kusomesha watoto, kuwapa huduma ya kliniki na kuimarisha kilimo.

Amesema kuwa mambo mengine ambayo walengwa wamenufaika nayo ni pamoja na uanzishaji wa biashara mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa imebadilisha maisha ya walengwa.

Naye Mkuu wa Msafara wa TASAF kutoka Makao Makuu Dkt. Jasson Bagonza alisema kuwa wako mkoani Tabora kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoratibiwa na Mfuko huo na kujadiliana na wadau mbalimbali ili kuona kama inakwenda malengo ya uanzishaji wake.

Amesema kuwa baada ya tathmini hiyo watakuja na TASAF awamu ya Tatu sehemu ya pili iliyoboreshwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na wananchi wake.

RC MAKONDA AWAKINGIA KIFUA VIONGOZI WA DINI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda amewataka Viongozi wa Dini zote Waislam na Wakristo wenye matatizo yanayohitaji msaada wa Serikali ikiwemo Migogoro na Kesi kufika Ofisi kwake ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

RC Makonda amesema hayo wakati wa Ibada ya uzinduzi wa Kanisa la KKKT Ubungo iliyoenda sambamba na Jubilee ya Miaka 500 ya Ujenzi wa Kanisa.

Amesema kuwa Viongozi wa Dini wanafanya kazi kubwa ya kiroho katika kuijenga Jamii Bora hivyo hawapaswi kuzungushwa na Watendaji wa Serikali pale wanapohitaji kuhudumiwa kwakuwa thamani ya kazi wanayoifanya ni kubwa.

Aidha RC Makonda amepongeza kanisa la KKKT Ubungo na washarika kwa Ujenzi wa Kanisa la Kisasa na kuwaomba kushirikiana katika kuijenga Dar es Salaam Mpya.

RC Makondaamewasihi Viongozi wa Dini kuendelea kuombea Taifa na Viongozi wake akiwemo Rais Dkt. Magufuli.

Kwa upande wake Askofu wa kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa amesema kazi anayofanya RC Makonda ni njema na inampendeza Mungu na kumtia moyo aendelee kuwatumikia Wananchi wa Dar es Salaam.

Katika ibada hiyo RC Makonda ameahidi kumnunulia Seti nzima ya Vifaa vya Mziki kwa mmoja wa Watoto katika kwaya ya Watoto katika kanisa hilo kwa kuonyesha kipaji cha kutumia vifaa hivyo kitendo kilichombariki RC Makonda.

SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA UMOJA WA MATAIFA

Serikali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na umoja wa mataifa katika kuleta maendeleo, katika sekta za kiuchumi na kijamii, kulinda amani, kuimarisha sekta ya viwanda na kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Karimjee na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kutimiza miaka 72 tangu kuanzishwa kwake.

Makamu wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu isemayo “Maendeleo ya viwanda na utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu,” alisema umoja wa mataifa umekuwa washirika wakubwa wa maendeleo katika sekta nyingi hapa nchini hususan maeneo ya vijijini katika huduma za maji, elimu pamoja na afya.

Aidha alisema kuwa katika kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 serikali inatoa wito kwa wadau wote na washirika wa UN kuja kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika kujenga viwanda, vilevile aliongeza kuwa uwepo wa amani, usalama pamoja na jitihada za vita dhidi ya ubadhilifu wa rasilimali, rushwa pamoja na urasimu ni nguzo kubwa ya wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.

Samia aliongeza kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na UN katika harakati za kulinda amani katika mataifa mbalimbali barani Afrika kama vile Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo. Vilevile alitoa wito kwa umoja huo kufanya mabadiliko katika baraza la usalama ili kuimarisha ulinzi, amani na ushrikiano dhidi ya makundi ya kigaidi yanayozidi kuongezeka kila uchao.

Kwa upande wake Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa, UN itaendelea kushirikina na Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linapita katika mabadiliko ya kiuchumi kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

“Wakati huu ambapo Tanzania inafanya mageuzi makubwa, inapoelekea kuwa nchi ya hadi ya kipato cha kati, msaada wa UN hauna budi kuendana na mahitaji na changamoto mpya, kwahiyo hatuna budi kuchukua mwelekeo mpya katika kazi. Kupitia malengo ya maendeleo endelevu, tutahakikisha kwamba hakuna mtu hata mmoja anayeachwa nyuma,” alisisitiza Rodriguez.

Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa aliongeza kuwa, kwa kushirkiana na serikali ya awamu ya tano UN watashawishi wadau na wawekezaji wengi kuja kusaidia shughuli za maendeleo ikiwemo kuwasaidia wakimbizi pamoja na kufadhili miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa viwanda, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuwawezesha na kuwalinda wanawake, watoto na vijana dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Sherehe ya kuadhimisha kuanzishwa kwa Umoja wa Matiafa imekuwa ikifanyika kila mwaka tarehe 24, Oktoba tangu kuanzishwa kwake mwaka1945 Jijini New York. Maadhimisho ya hivi karibuni yamekuwa yakitilia mkazo maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya viwanda.

Kwa sasa UN hapa nchini inatekeleza mpango uliozinduliwa hivi karibuni kwaajili ya Mkoa wa Kigoma (The Kigoma Joint Programme) ambao utatekelezwa kati ya 2016-2021 katika Wilaya tatu za Kasulu, Kibondo na Kakonko pamoja na mkakati wa maendeleo endelevu kwa ustawi wa watu na uhifadhi wa mazingira.

Page 7 of 168