blog category

WANANCHI WA MANISPAA YA MTWARA MIKINDANI WAHIMIZWA UTUNZAJI WA MIFEREJI

Wananchi na wafanyabiashara waliopo Manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kutupa taka taka katika mifereji iliyopo pembezoni mwa barabara ambayo hutumika kusafirishia maji kuelekea baharini.

Hayo yamebainishwa na Afisa habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bi.Jamadi Abdallah wakati akizungumza na Safari Media na kusema kuwa kumekuwa na tabia mbaya ya wananchi na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitupa taka taka katika mifereji jambo ambalo ni hatari ambalo huepelekea mifereji kuziba na hatimae kusababisha mafuriko

Hata hivyo kutokana na utabiri uliotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini imeweka wazi kuwa mvua zitakuwa nyingi na za kutosha na ukizingatia tunaelekea katika msimu wa mvua za masika hivyo ni muhimu wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira

Sanjari na hayo Bi. Jamadi amewataka kila mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake ili kuhakikisha hakuna anyekiuka sheria kwa kutupa taka taka katika mifereji

TUMIENI MALIGHAFI ZA NCHINI KATIKA VIWANDA VYENU- MAKAMU WA RAIS

Serikali imezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumia malighafi zinazopatikana katika nchi hizo kwa ajili ya viwanda badala ya kuagiza nje.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Biashara na Ujasiriamali ya Afrika Mashariki.

Makamu wa Rais amewataka wakulima waongeze thamani ya mazao yao badala ya kuuza mazao ghafi, Kwa kufanya hivyo watajiongezea kipato na kuondokana na umaskini, aliongeza Samia.

Uanzishwaji wa viwanda katika Jumuiya ya Afrika mashariki utasaidia katika kuinua kilimo kwani mazao hayo yatapata uhakika wa soka kwenye viwanda hivyo.

Amezitaka nchi hizo kutengeneza ajira hasa kwa vijana ambao takwimu zinaonyesha kuwa ndio wengi, hivyo ni muhimu kuwapa kipaumbele.

Serikali na sekta binafsi zimetakiwa kufanya juhudi za makusudi kuanzisha viwanda ambavyo vitaongeza ajira na kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.

Aidha, Mhe. Samia amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kudumisha amani kwani bila amani uwekezaji katika viwanda na maeneo mengine hauwezekeni.

Amani ni bidhaa adimu ambayo inapatikana kwa gharama, hivyo siyo ya kuchezea bali ni ya kulindwa, aliongeza Mhe. Samia.

Huu ni Mkutano wa Pili ambao unajumuisha washiriki kutoka, Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda na wenyeji Tanzania. Katika Mkutano huo yanafanyika maonyesho ya wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki.

KILIMO WATAKIWA KUTAFITI MBEGU BORA ZA PAMBA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina ili kupata aina bora ya mbegu za pamba zitakazowanufaisha wakulima.

Amesema ni lazima utafiti huo ufanyike kwa kuzingatia aina ya udongo unaopatikana katika kila mkoa unaolima pamba.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Novemba 14, 2017) alipozungumza na wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima pamba, Bungeni mjini Dodoma.

Amesema Wizara ya Kilimo itumie taasisi zake vikiwemo vyuo kufanya uchunguzi na kubaini ni aina gani za mbegu zinafaa kutumika kulingana na eneo husika.

Amesema utafiti huo ambao utabainisha aina ya mbegu inayofaa kulingana na aina ya udongo katika kila eneo ili kumuwezesha mkulima kupata mazao ya kutosha.

Pia aliwataka Maofisa Kilimo katika mikoa inayolima mazao makuu ya biashara waweke kipaumbele katika kuyasimia mazao hayo.

Waziri Mkuu amesema Maofisa hao lazima wahakikishe wanayasimamia vizuri mazao hayo ambayo ni korosho, chai, pamba, kahawa na tumbaku ili yawe na tija.

Alisema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.

Waziri Mkuu alisema Serikali inataka kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.

“Tunataka kulifanya zao hilo ambalo lilikuwa likijulikana kama dhahabu nyeupe lifikie kiwango cha juu cha uzalishaji, hivyo kuongeza tija kwa wakulima.”

Pia Waziri Mkuu aliwaagiza Maofisa Kilimo katika mikoa hiyo wafanye sensa ili kutambua idadi ya wakulima wa pamba na ukubwa wa mashamba yao.

Alisema lengo la sensa hiyo ni kutambua idadi ya wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kurahisisha usambazaji wa pembejeo kulingana na mahitaji.

Wakizungumza katika mkutano huo baadhi ya wabunge waliiomba Serikali kuhakikisha zao hilo linaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuwafikishia wakulima pembejeo kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa Itilima Bw. Njalu Silanga aliiomba Serikali izibane Halmashauri ili kuhakikisha fedha za miradi ya kilimo zinatumika ipasavyo.

Bw. Silanga alisema msukumo wa Serikali wa kufufua zao la pamba umeanza kuzaa matunda, hivyo aliiomba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutafuta masoko ya kutosha.

Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Bi Ester Matiko ameiomba Serikali kuwaelimisha wananchi na kuwahamasisha kulima kilimo hicho ili waachane na kilimo cha bangi.

Bi. Ester amesema kati ya mazao makuu matano ya biashara manne yanalimwa katika jimbo lake ambayo ni chai, pamba, kahawa na tumbaku, hivyo wakulima wakipewa elimu ya kutosha juu za mazao hayo watapata tija.

BYAKANWA AANZA KUTEMA CHECHE MTWARA

Watendaji wa Serikali Mkoani Mtwara wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu wanapo tekeleza majukumu yao ya kila siku ili kufikia malengo ya adhma ya Serikali ya awamo ya tano ya uchumi wa Viwanda

Wito huo umetolewa mapema hii leo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa wakati wa makabidhiano ya ofisi yake kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Mstaafu Bi Halima Dendego, ambapo amesema kuwa endapo watendaji wa Serikali watatekeleza hayo itasaidia kuondoa malalamiko yasiyo ya Msingi na watafikia haraka malengo yao.

Aidha amesema kuwa endapo wakizingatia uongozi wa Sheria watamaliza migogoro ya Ardhi na kukaa kushughulikia maswala muhimu ya maendeleo ya Mtwara.

Mh Byakanwa amekiri kupokea changamoto zilizopo mkoani Mtwara na Miradi inayo tekelezwa hivi sasa na kuahidi kuanza kusimamia swala la elimu ambalo mkoa wa Mtwara uko nafasi ya 22 kitaifa kati mikoa 26 kwa matokea ya Darasa la saba mwaka huu 2017.

Amesema kuwa hatokubali kuona mkoa huo unaingia katika orodha ya mikoa 10 ya mwisho na badala yake anataka uingia katika nafasi ya mikoa mitano ya kwanza kitaifa.

Kwa upande wake Bi Dendego amewaomba watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya wampatie ushirikiano kama walivyo mpatia yeye ili kuweza kufikia mafanikio.

Ikumbukwe kuwa Dendego wakati anaingia mkoani Mtwara mwaka 2014 kulikuwa na hali haikuwa shwari kutokana na vuguvugu la Gesi na anaicha Mtwara katika hali ya amani na utulivu.

WAJUMBE WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE MASUALA YA UKIMWI WAJENGEWA UWEZO

Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Taifa yakudhibiti Ukimwi (TACAIDS) imedhamiria kuendelea kuwajengea Uwezo Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inashughulikia Ukimwi ili iweze kushiriki vyema katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Akizungumza wakati wa Semina ya siku tatu iliyoanza leo mjini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vita dhidi ya janga la Ukimwi inafanikiwa ili kulinda nguvu kazi ya Taifa.

“Serikali imejipanga kuhakikisha swala hili linapewa kipaumbele hasa katika kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI,” alisisistiza Mhe. Mhagama

Akifafanua Mhe. Mhagama amesema kuwa vita dhidi ya janga la Ukimwi niya kila Mtanzania hivyo ni vyema wadau wote wakashirikiana na Serikali katika mapambano hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inashughulikia Ukimwi Mhe. Daniel Mtuka amesema Warsha hiyo inajenga msingi kwa wajumbe wa Kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

Aliongeza kuwa Wajumbe wa Kamati hiyo wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na Ukimwi hapa nchini ili kuhakikisha kuwa malengo yakuondoa janga hilo hapa nchini yanatimizwa kwa wakati muafaka.

Kwa Upande wake mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Mhe. Martha Mlata amesema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa jamii kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya Janga la Ukimwi kwa kusimamia maadili katika Jamii hali itakayochochea kuleta mabadiliko.

Warsha ya Siku tatu kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inashughulikia Ukimwi inafanyika mjini Dodoma kwa siku tatu ikilenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

KATIBU MKUU MPYA WA MADINI ATEMA CHECHE

Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, amewataka watumishi wa Wizara kuwajibika katika nafasi zao ili wananchi wanufaike na matunda ya kazi zao kama inavyopaswa.

Profesa Msanjila aliyasema hayo jana, Oktoba 30, 2017 baada ya kuwasili rasmi Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma na kupata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi.

Amefafanua kuwa, uwajibikaji hupimwa kwa matokeo. “Tutakuuliza umefanya nini katika nafasi yako ili tuweze kupima utendaji wako.”

Aidha, Profesa Msanjila alisisitiza ushirikiano baina ya viongozi na wafanyakazi wote ili kupata matokeo chanya, hivyo kuleta manufaa katika sekta ya madini.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara ya Madini, Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, aliahidi ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi na uwajibikaji katika nafasi zao kama alivyoasa Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu Msanjila, alipokelewa na watumishi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Lusias Mwenda.

KODI YA MAJENGO YAFIKIA BILIONI 34.09 MWAKA 2016/17

Serikali imesema makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yanayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.28 mwaka 2015/16 hadi Bilioni 34.09 kwa mwaka 2016/17.

Akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mhe. Wilfred Lwakatare Bungeni Mjini Dodoma aliyedai kuwa kuna athari za kuhamishwa kwa tozo ya kodi ya umiliki wa nyumba kutoka Serikali za Mitaa kwenda TRA, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesmea kuwa hatua hiyo haijaathiri mapato bali uamuzi huo umesaidia kuongeza mapato hayo.

“Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma na maendeleo kwa wananchi.

Hata hivyo, hatua ya Serikali kukasimu jukumu la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa TRA haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali kuimarisha ukusanyaji wake,” alisema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji amesema, kumekuwepo na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa kodi ya majengo pamoja na matumizi ya mapato yanayotokana na kodi hiyo.

Aidha amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ufanisi katika ukusanyaji na matumizi ya kodi zote zinazokusanywa ndani ya Taifa. Halmashauri zote zitapata mgawo wa fedha kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya Serikali.

Ameendelea kwa kusema kuwa, makusanyo yatokanayo na kodi ya majengo yameongezeka kwa asilimia 20.6 ya makusanyo halisi yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa TRA mwaka wa fedha 2016/17.

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18 (Julai – Septemba) TRA ilipangiwa kukusanya kodi ya majengo ya kiasi cha shilingi bilioni 11.9. Hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu TRA ilifanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 13.2 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 111.

POLEPOLE ANENA KUHUSU NYALANDU

Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM , Humphrey Polepole amesema uamuzi uliochukuliwa na Mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM, Lazaro Nyalandu wa kujivua uanachama wa chama hicho na ubunge ni jambo la kawaida.

Polepole ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na Safari Radio na kusema CCM inatambua haki za msingi za kila raia na uamuzi wa Nyalandu kujivua uanachama kwao walipokea kama habari ya kawaida lakini pia ni afya kwa demokrasia ya nchi.

Nyalandu ametangaza uamuzi wa kujivua uanachama wa CCM na ubunge jana jumatatu ya Oktoba, 30 na kuomba Chadema kumpa nafasi ya kujiunga na chama hicho, ombi ambalo limejibiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kumwambia kuwa milango ipo wazi.

Page 6 of 168