blog category

TANESCO WALALAMIKIWA KWA KUTELEKEZA NYAYA, NGUZO ZA MRADI WA KIFURU

Wakazi wa Kata ya Kinyerezi eneo la Kifuru kwa Kinana wameulalamikia uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kituo cha Tabata jijini Dar es Salaam kwa kitendo cha kutelekeza nguzo na nyaya za mradi wa umeme eneo hilo ambapo zimegeuka kero.

Wakizungumza eneo hilo kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wakazi hao, wamesema TANESCO kituo cha Tabata walileta nguzo na nyaya tangu mwaka jana na kuziweka barabara inayoelekea King’azi (Kwa Godoro) Mtaa wa Tanganyika ambapo baada ya mvua za mwishoni mwa mwaka jana 2017 baadhi ya nguzo zilianguka na nyaya kutandaa chini jambo ambalo limekuwa kero baada ya kuziba barabara ya mtaa huo na magari kupita kwa taabu.

Mkazi wa Mtaa wa Tanganyika, Rashid Abdallah alisema mradi huo umechukua zaidi ya miaka miwili sasa huku wateja walioomba umeme eneo hilo wamekuwa wakizungushwa kwamba wasubiri mradi huo bila ya mafanikio.

Alisema kwa sasa wamekuwa kama walinzi wa nguzo na nyaya hizo za TANESCO mtaani hapo maana wanahofia zikiibiwa huenda matumaini ya mradi huo wanaoahidiwa kila kukicha kukamilika ukatoweka kabisa.

Kwa upande wake mkazi mwingine wa eneo hilo, Senzekwa Magila alisema wanashangaa kuzungushwa maombi yao ya kufungiwa umeme wakielezwa kusubiri mradi ambao haukamiliki ilhali wanaendelea kutaabika. Alisema TANESCO inapaswakujifunza na kuwa makini kwa uongozi wa sasa kwani unahimiza uchapaji kazi bora unaolenga kuiingizia Serikali na taasisi zake mapato ya kutosha, jambo ambalo wanashangaa wateja wanaomba huduma zaidi ya miaka miwili bila mafanikio.

Naye mkazi mwingine ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kinachowakaza zaidi ni kitendo cha maeneo yote yaliozunguka mtaa huo kuunganishwa umeme lakini wao Mtaa wa Tanganyika hadi leo wamekuwa wakipigwa danadana bila mafanikio.

Alisema wengi wao wamejinyima na kuanza kufunga mfumo wa umeme mapema katika nyumba zao lakini hadi leo hawajaunganishwa.

KIGWANGALLA ATISHWA NA WAHALIFU

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema wahalifu wanazidi kubuni mbinu mpya baada ya kubaini ubora wa mifumo ya kiintelijensia inayotumiwa na wizara yake kubaini uhalifu dhidi ya raslimali.

Waziri Kigwangalla amesema hayo baada ya operesheni kwa kutumia Intelijensia (intelligence-led operations) kufanikisha kukamatwa kwa Lori la kubeba mawe ya gypsum ambalo lilikwa limebeba mbao zilizopatikana kwa njia zisizo halali.

Ijumaa ya tarahe 26/11/2017 majira ya asubuhi Lori lenye namba za T862 BTZ na tela lenye namba T545 BLA, mali ya kampuni ya Swift Motors, likiendeshwa na Bw.

Baraka Jackson lilikamatwa likiwa limebeba mbao huku zikiwa zimefichwa na mawe ya Gypsum, katika kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu cha Kiranjeranje wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi.

Hata hivyo waziri Kigwangalla amesema mifumo ya kisasa ya Kiintelijensia inayotumiwa na wizara yake inatuwezesha kukamata wahalifu wa raslimali na mazao ya misitu kwa ujumla.

WADAIWA WA HESLB WAANZA KUSAKWA.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatarajia kuanza kuwasaka jumla ya wanufaika 119,497 nchini kote ambao wamekiuka sheria iliyoanzisha Bodi hiyo kwa kutoanza kurejesha mikopo yenye thamani ya TZS 285 bilioni waliyokopeshwa tangu mwaka 1994/1995 na mikopo yao imeiva lakini hawajaanza kurejesha.

Aidha, Bodi ya Mikopo inatarajia kuanza kufanya ukaguzi kwa waajiri mbalimbali nchini kote ili kubaini kama katika orodha za waajiriwa wao kuna wanufaika wa mikopo ambao hawajaanza kurejesha.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema jijini Dar es Salaam kuwa msako huo utafanywa kwa miezi mitatu kuanzia wiki ijayo (Jumatatu, Januari 8, 2018).

Bw. Badru ametoa kauli hiyo wakati akitoa tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Mikopo kwa nusu ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 uliomalizika Desemba 31, 2017

Katika tathmini hiyo, Bw. Badru alizungumzia mafanikio, changamoto na mipango ya kuboresha ufanisi katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva.

Maafisa wa Bodi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali wamejipanga katika kutekeleza hili ili kuongeza makusanyo ya mwezi kutoka wastani wa TZS 13 bilioni hivi sasa hadi kufikia TZS 17 bilioni mwezi Juni, 2018.

Orodha kamili ya waajiri na wanufaika wa mikopo ambao wanakiuka Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa kutowasilisha makato au kurejesha mikopo ya elimu ya juu inapatikana katika tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) kuanzia jana (Jumatano, Januari 3, 2018).

Akifafanua zaidi, Bw. Badru amesema ingawa kila mwajiri ana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha makato ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kwa Bodi ndani ya siku 15 baada ya mwisho wa mwezi, baadhi ya waajiri wamekuwa hawafanyi hivyo na kuilazimisha Bodi ya Mikopo kuanza kuwasaka kwa nguvu.

Akizungumza kuhusu hali ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva hadi kufikia Desemba 31, 2018, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kiasi cha TZS 85 bilioni kilikuwa kimekusanywa huku lengo la makusanyo kwa mwaka mzima wa fedha utakaomalizika Juni 30, 2018 ni TZS 130 bilioni.

Kuhusu changamoto inayokutana nazo katika kazi ya ukusanyaji wa mikopo, Bw. Badru amesema baadhi ya waajiri kutowasilisha kwa Bodi ya Mikopo orodha za waajiriwa ambao ni wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kama sheria inavyotaka. Aidha, changamoto nyingine ni kutowasilisha makato ya wanufaika kwa Bodi kwa wakati.

Hali ya Utoaji Mikopo kwa Mwaka 2017/2018

Kuhusu utoaji mikopo kwa wanafunzi wahitaji, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema katika mwaka huu wa masomo, jumla ya wanafunzi 122,623 wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 422.45 bilioni. Kati yao, wanafunzi 33,244 ni wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 110.37 bilioni na wengine 89,379 ni wanaoendelea na masomo ambao wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 312.16 bilioni.

Katika mwaka wa masomo uliopita (2016/2017), jumla ya wanafunzi 112,409 walipangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 409.61 bilioni. Kati ya hao, wanafunzi 28,383 walikuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 86,688 walikuwa wanaendelea na masomo.

Bodi ya Mikopo ilianzishwa kwa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005. Majukumu makuu ya Bodi ya Mikopo ni kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji wenye sifa na kukusanya mikopo iliyoiva ili iweze kukopeshwa kwa wahitaji.

NHC YATOA KIWANJA KWA JESHI LA POLISI ARUSHA KWA AJILI YA UJENZI WA KITUO

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 5000 kwa Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi na nyumba za askari katika eneo la Matevesi ambapo kuna mradi wa Safari City umbali wa kilomita 12 kutoka katikati ya mji wa Arusha.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Masoko wa Shirika hilo nchini Bw. Itandula Gambalagi alisema kwamba, wanatambua umuhimu wa Usalama ndio maana wameamua kutoa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi pamoja na makazi ya askari.

Alisema uwepo wa Jeshi la Polisi katika eneo hilo utawavutia wawekezaji na wakazi wa eneo hilo kuwa na uhakika wa usalama wao na kuliomba Jeshi hilo kuanza kufanya maandilizi ya ujenzi wa kituo hicho kabla ya makazi na maeneo ya biashara hayajafunguliwa.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba Jeshi hilo litachukua hatua za mapema ili kuweza kujenga kituo hicho ambacho kitaimarisha usalama katika eneo hilo.

“Watu wanaotaka kuwekeza katika eneo hilo wasiwe na shaka juu ya hali ya usalama lakini pia kituo hicho kitasaidia wakazi wa maeneo jirani na kiwanda cha A to Z kilichopo kilomita kadhaa kutoka katika kituo hicho,” alisisitiza Kamanda Mkumbo

Naye Meneja Mradi wa Safari City Bw. James Kisarika alisema kwamba mbali na maeneo ya makazi pamoja na biashara lakini pia wametenga maeneo kwa ajili ya huduma za jamii kama vile viwanja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, Misikiti, Makanisa, Shule za Sekondari na Msingi, kituo cha mabasi madogo pamoja na viwanja vya Michezo.

JESHI LA POLISI SINGIDA LAKAMATA KILO 100 ZA BANGI

Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, limetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wa madawa ya kulevya kwamba mkoa huo sio eneo salama kwa ajili ya kupitisha madawa ya kulevya.

Onyo hilo limetolewa na Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, Mrakibu Mwandamizi Isaya Mbugi, wakati akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari juu ya msako mkali unaoendelea katika kupambana na vita ya madawa ya kulevya mkoani humo.

Amesema kuwa ni muda sasa wameanzisha msako wakishirikisha mbwa wenye utaalamu wa hali ya juu, kwa ajili ya kukamata wafanyabiasha na watumiaji wa madawa mbalimbali ya kulevya.

Amesema katika msako huo walioufanya leo Januari 3, 2018, walifanikiwa kukamata madawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 100.

Kaimu kamanda huyo, alisema wamefanikiwa kukamata basi hilo la Kisobo, kwa lengo ya kumkamata mfanyanyabishara huyo wa madawa ya kulevya.

Kwa kutumia mbwa, Jeshi la Polisi mkoani hapa, hivi karibuni, lilifanikiwa kukamata madawa ya kulevya aina ya horoine gramu 80 na misokoto ya bhangi 40.

NAIBU WAZIRI WA MAJI AKATAA KUWA WA MWISHO

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesisitiza kuwa wizara yake haitakuwa kikwazo cha utekelezaji wa ahadi ya Rais, Dkt. John Magufuli ya kuwapatia wananchi majisafi na salama, bali itasimimamia utekelezaji wa miradi hiyo ipasavyo ili ikamilike kwa wakati na kuleta tija.

Aweso amezungumza hayo katika ziara yake ya kikazi aliyoianza katika mkoa wa Ruvuma, ambapo anakagua utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya zote mkoani humo.

‘‘Niwahakikishieni wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini, zaidi ya kuhakikisha miradi yote tunayoitekeleza inaleta tija na kumaliza kero ya maji kwa wananchi kulingana na maagizo ya Rais.

Hivyo, lazima fedha zifike kwa wakati na zitumike kwa usahihi ili miradi yote ikamilike kwa wakati kulingana na mikataba,’’ alisema Naibu Waziri.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji ametoa pongezi kwa SOUWASA kwa usimamizi mzuri wa miradi na hatua inazozichukua kwa nia ya kumaliza kero ya maji katika maeneo ya mji huo kama Midizini na Misufini ambayo yalikuwa na kero kubwa, lakini kwa sasa wananchi kukiri kupata huduma hiyo.

Katika ziara hiyo ameanza kwa kutembelea Wilaya ya Songea, ambapo ametembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Songea (SOUWASA) na kuweza kuzungumza na menejimenti yake, pamoja na watumishi.

Aidha, alitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika wilaya hiyo ikiwemo eneo la mradi wa Bwawa la Luhira, mtambo wa kutibu na kusafishia maji wa Matogoro, mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi Songea.

Huduma ya maji kwa mji wa Songea kwa sasa ni asilimia 79, ambapo lita milioni 10.6 zinazalishwa kwa siku na mahitaji yakiwa ni lita milioni 14 kwa siku kwa wakazi wa mji huo.

Upanuzi wa mradi wa maji wa Songea mjini unaondelea hivi sasa unategemea kuongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 90 kwa mji wa Songea.

TRA KUONGEZA IDADI YA WALIPA KODI

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa inatarajia kusajili walipakodi wapya takribani 1000,000 ambao kwa pamoja wanakadiriwa kuwa wataongeza mapato ya tokanayo na kodi kwa kiwango cha Sh. Bilioni 1.5 kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa zoezi la usajili wa wafanyabiashara wadogo zoezi lilionza katika Eneo la Chanika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya amesema kuwa kampeni ya kusajili wafanyabiashara wadogo ni endelevu.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Richard Kayombo ameelezea jambo mbele ya Waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa na Utoaji wa Namba za Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) lililofanyika katika eneo la Chanika, Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Aidha Mwandumbya alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili waweze kusajiliwa kama walipa kodi na kupatiwa Namba za Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN).

Amesema kuwa uhamasishaji wa ulipaji kodi na usajili utaendelea kwa kuweka vituo karibu na wafanyabiashara.

Aidha Kayombo amesema, Mamlaka hiyo imeamua kuja na kampeni hii baada ya kutambua kuwa kulikuwa na usumbufu kwa wafanyabiashara kupata TIN namba, kutokana na umbali kutoka wakazi wa eneo hilo hadi Vingunguti.

Pamoja na hayo amewatahadhalisha wananchi kutolaghaiwa na matapeli kwani kazi hiyo inafanya na TRA yenyewe na hakuna wakala aliye pewa kazi hiyo.

MAWAZIRI WANNE WA UGANDA WAFANYA ZIARA NCHINI

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amekutana na mawaziri wanne kutoka nchini Uganda ambao wamewasili nchini Tanzania kwa ajili ya ziara ya siku mbili ya kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa Sekta ya Madini.

Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi- Madini, Lokeris Peter, Waziri wa Nchi- Mambo ya Ndani, Obiga Kania, Waziri wa Nchi- Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala, Namugwanya Bugembe na Waziri wa Nchi- Masuala ya Uchumi, Dkt. Kasirivu Atwooki.

Waziri Kairuki amekutana na ujumbe huo Novemba 28, 2017 katika Ofisi za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam na kujadiliana masuala mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za Madini nchini ikiwemo suala la Sera, Sheria na Kanuni za Madini pamoja na masuala yanayohusu Wachimbaji Wadogo wa madini.

Majadiliano baina ya Wizara na Ujumbe huo vilevile yalihusisha uwasilishaji wa mada mbalimbali kutoka kwa Kamishna wa Madini, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Ujumbe huo utatembelea migodi mbalimbali ya Dhahabu inayomilikiwa na wazawa iliyoko mkoani Geita ili kujionea uendeshaji wa migodi hiyo na hivyo kupata uzoefu wa namna ya uendeshaji wake.

Aidha, ujumbe huo wa Mawaziri kutoka nchini Uganda, utatembelea nchi mbalimbali Barani Afrika ili kupata uzoefu wa usimamizi wa Sekta ya Madini hususan suala la Wachimbaji Wadogo.

Page 4 of 168