blog category

MKUTANO WA KUJADILI NAMNA YA KUONGEZA PATO LA TAIFA WAFANYIKA MWANZA

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameongoza Mkutano mkubwa wa wadau wote wa madini katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa uliojadili namna ya kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa pamoja na udhibiti wa utoroshaji wa madini.

Mkutano huo umefanyika jijini Mwanza, umeazimia kwa sauti moja kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi.

Aidha, Mkutano umependekeza kuwepo na Mnada au Soko la pamoja la Madini ya Dhahabu ili kuweka mazingira wezeshi na yenye tija kwa wadau wote wa sekta hiyo.

Kufuatia maazimio hayo, Mkutano uliunda Kamati yenye wajumbe 14 kutoka kada mbalimbali za sekta husika, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa sasa wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina na Katibu ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria – Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba.

Akiwasilisha Hadidu za Rejea kwa Kamati husika ambayo imeahidi kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya siku 30 kuanzia jana Februari 25, Mwenyekiti wa Mkutano ambaye ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alizitaja kuwa ni pamoja na kuainisha utaratibu utakaotumika kuanzisha Soko hilo la Dhahabu katika Jiji la Mwanza kama ilivyopendekezwa.

Ametaja kazi nyingine inayopaswa kufanywa na Kamati hiyo kuwa ni kubainisha mbinu zitakazotumika kupata washiriki wa Mnada huo ikiwa ni pamoja na wauzaji na wanunuzi.

Aidha, Kamati imetakiwa kuandaa na kuwasilisha Mkakati utakaobainisha utaratibu mzima au mbinu sahihi zinazopaswa kutumika katika zoezi zima la kuanzia ununuzi hadi upatikanaji wa kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi kwa kutumia muda mfupi.

Kazi nyingine ya Kamati husika ni kupambanua faida na hasara za uwepo wa Soko hilo ili kuleta uelewa kwa wadau wote wanaohusika.

Awali, akizungumza katika Mkutano huo, Naibu Waziri alisema kuwa kwa niaba ya Serikali, ameafiki mapendekezo ya wajumbe na utayari wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kutoa eneo katika Jiji lake kwa ajili ya kufanyikia kwa Mnada husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alimhakikishia Naibu Waziri na wadau wote kuwa Ofisi yake iko tayari kutoa eneo zuri na salama kwa ajili ya kuendeshea Mnada husika.

Akizungumza katika Mkutano huo, Rais wa FEMATA, John Bina aliwaasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia haki na wajibu wao kama sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya madini zinavyoelekeza ili kufanikisha maazimio ya Mkutano huo kuhakikisha suala la utoroshaji madini linakoma.

Awali, akizungumzia lengo la kuandaa Mkutano huo, Kamishna Msaidizi wa Kanda, Mhandisi Samamba alibainisha kuwa ni kutokana na changamoto ambayo imeibuka ya utoroshaji wa madini.

Kabla ya kufikia maazimio husika, asilimia kubwa ya wajumbe wa Mkutano huo walikiri kuwa utoroshaji wa madini upo ambapo kwa madai yao, hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na utozwaji wa kodi na tozo mbalimbali stahiki.

Waliiomba Serikali ipunguze kodi na tozo zilizopo ili waweze kumudu kuzilipa na hivyo kuachana na udanganyifu wa aina mbalimbali unaoendelea katika sekta hiyo.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Mhandisi Samamba alifafanua kuwa, suala la kulipa kodi limekuwa ni changamoto kwa wachimbaji wengi kutokana na kushindwa kutunza kumbukumbu zao hivyo kulazimika kulipa zaidi tofauti na wale wanaomudu kutunza kumbukumbu zao ambao hujikuta wanalipa kodi kidogo.

Vilevile, walitaja changamoto ya Soko la uhakika linalosababishwa na wengi wao kutokufahamu bei halisi ya dhahabu na ndiyo sababu wengi wakapendekeza kuanzishwa kwa Soko la Pamoja.

MKURUGENZI MTWARA AFAFANUA TAARIFA ZA UCHANGIAJI ELIMU

Mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani Bi. Beatrice Dominic Kwai, amekanusha taarifa za kuchangia elimu, wafanyakazi wa manispaa hiyo.

Mkurugenzi huyo amesema yeye binafsi hajatoa taarifa yoyote kuomba wananchi wala wafanyakazi wa manispaa hiyo kuchangia elimu, kwani kufanya hivyo ni kukiuka agizo la Rais la kutaka elimu itolewe bure.

"Sina taarifa na hilo, ninachojua mifuko ya elimu ipo kisheria na wa kwangu tunajiandaa kuuzindua, kwakuwa sina document yoyote niliyosaini inayohusiana na michango, na mimi ninatambua maagizo ya Mheshimiwa Rais, siwezi kuchagisha michango ambayo ipo kinyume na utaratibu na sijamuagiza mtu yeyote achangishe", amesema Beatrice.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kuwa wananchi wa Manispaa hiyo pamoja na wanafunzi wametakiwa kuchangia elimu kiasi cha shilingi elfu 5 kila mmoja, jambo ambalo lipo kinyume na agizo la Mheshimiwa Rais Magufuli.

WAZIRI MKUU AZINDUA MRADI WA MAJI UKEREWE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji katika kijiji cha Bwasa katika mji wa Nansio wilayani Ukerewe na kuuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha maji hayo yanatoka wakati wote na mradi huo unakuwa endelevu.

Waziri Mkuu amezindua mradi huo jana wakati akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Alisema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini.

Baada ya kuzindua mradi huo, Waziri Mkuu amezungumza na wananchi wa mji wa Nansio kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Getrude Mongella, ambapo alisema mradi aliouzindua katika kijiji cha Bwasa ni sehemu ya mradi wa maji wa Kazilankanda utakaohudumia vijiji 13 vya wilaya hiyo.

Amesema mradi huo unagharimu shilingi bilioni saba na unatekelezwa katika vijiji vya Muhula, Mahande, Namasabo, Namagondo, Kazilankanda, Malegea, Igalla, Kigara, Lutare, Busunda, Bwasa, Buhima, Hamuyebe na utahudumia wakazi 68,038 pindi utakapokamilika.

Mkataba wa Mradi huo ulisainiwa Machi 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo April, 2018, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 5.637 sawa na asilimia 78.26 tayari zimeshatumika na mradi umekamilika kwa asilimia 92 na tayari baadhi vijiji vimeanza kupata maji.

Waziri Mkuu amesema mkakati wa Serikali ni kuwahudumia wananchi kwa kutatua kero zinazowakabili ikiwemo ya upatikanaji wa maji, ambapo imedhamiria kuendelea kusambaza huduma hiyo hadi vijijini ili kuhakikisha vyote vinapata maji.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Waziri Mkuu amewaambia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta maji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Bw. Estomihn Chang’ah apange siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hususani za ardhi na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu huyo wa wilaya leo saa 3.00 asubuhi akiwa na watumishi wa Idara ya Ardhi akutane na wananchi wote wenye malalamiko ya ardhi ili ashirikiane nao katika kuyapatia ufumbuzi. Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko mengi ya wananchi yahusuyo masuala ya ardhi yaliyowasilishwa kwake kupitia njia ya mabango.

Amesema kwa sababu ya kutotekeleza wajibu wao ipasavyo kumekuwa na kero na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na hivyo kusababisha wananchi kuwasilisha kero na malalamiko hayo wakati wa ziara za viongozi wakuu wa nchi.

TBA YATAKIWA KUJITATHMINI UBORA WA JENGO LA FORODHA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Elius Mwakalinga akafanye tathmini ya ubora ya jengo la kituo cha pamoja cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.

Ametoa agizo hilo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo alimuagiza Mkurugenzi huyo afanye tathmini na kuishauri Serikali kama jengo linafaa kutumika.

Januari 17, 2018 Waziri Mkuu alikagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo alisema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango.

Pia Waziri Mkuu alipokagua jengo hilo alijionea mwenyewe kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu miradi ya maji inayotekelezwa katika mkoa huo, ambapo alisema “Miradi mingi ya maji mkoani Mara ni ya hovyo na fedha nyingi zimetumika na wananchi hawajapata huduma hiyo.”

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaelekeza viongozi wa mkoa huo ifikapo Januari 25, 2018 wamkabidhi taarifa ya mikakati waliyonayo ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi.

ACT WAZALENDO YATAKA WAZIRI NCHEMBA NA IGP SIRRO WAJIUZULU

Kufuatia kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline, Chama cha ACT-Wazalendo kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba awajibike kwa kujiuzulu wadhifa wake, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro wajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT, Licapo Bakari amesema chama hicho kina laani vikali mauaji ya Akwilina.

Amesema, viongozi hao wamekuwa kimya na kutochukua hatua pindi mauaji ya watu wasio na hatia yanapotokea kwa ajili ya kuyatokomeza.

Aidha, Bakari amesema ACT inataka uchunguzi huru ufanyike kuhusu tukio hilo pamoja na matukio mengine yaliyotokea awali ufanyike.

WAZIRI KIGWANGALLA KUWA MGENI RASMI ONESHO LA CHIMBUKO LA BINADAMU AFRIKA,DAR

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi leo Januari 23.2018, kwenye uzinduzi wa Onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika, tukio ambalo litafanyika majira ya saa 11 jioni katika viunga vya Makumbusho ya Taifa, yaliyopo mtaa wa Shabani Robert, mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Akizungumza wakati wa utambulisho wa tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla amebainisha kuwa, tayari maandalizi ya onesho hilo yameenda sawa na watu mbalimbali watanatarajiwa kushuhudia tukio ambalo ni la siku moja wakiwemo viongozi wa Serikali na Mabalozi waliopo nchini, na watalii wanatarajiwa kuhudhuria.

Profesa Mabulla amebainisha kuwa, Vioneshwa vyote katika onesho hilo hapo kesho, vimepatikana hapa Tanzania kutokana na tafiti za kisayansi na vimehifadhiwa Makumbusho ya Taifa.

Kwa upande wake Mratibu kwa upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna amesema Onesho limegawanyika katika sehemu kuu nne zikiwemo Makumbusho ya Taifa la Tanzania ikishirikiana na Ubalozi wa Spain Tanzania.

Hii ni pamoja na Makumbusho ya Akiolojia ya Madrid, Taasisi ya Chimbuko la Binadamu (IDEA) Madrid, Chuo Kikuu cha Alcala Madrid na Makumbusho ya CosmoCaixa Barcelona-Spain huku tamasha zima likidhaminiwa na Kampuni ya Simenti ya Twiga.

Aidha Dk.Agness ameongeza kuwa, Onesho hilo litakuwa katika pande nne ikiwemo sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dkt. Mary D. Leakey. Nyayo hizo ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ni ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopia.

Sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo) ambapo kuna masalia ya zamadamu Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo (Oldowan) zilizotumika katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.

Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus. Jamaii hii inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kuna masalia ya zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile tembo na nyati wa zamani takribani miaka million 1.7 iliyopita.

Sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Kuna masalia ya Homo sapiens na zana za mawe za muhula wa kati na muhula wa mwisho.

Mbali na onesho hilo, pia waandaji hao wa Makumbusho ya Taifa inawakaribisha watu wote kuhudhuria semina na ufunguzi wa onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika.

SERIKALI KUCHUNGUZA KIFO CHA MWANAFUNZI ALIYEPIGWA RISASI

Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya uchunguzi kufuatia kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Baftaha Akwilini, aliyefariki kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni amesema kuwa Serikali itahakikisha uchunguzi huo unafanyika kwa weledi na utaalamu ili haki iweze kupatikana na yeyote aliyehusika atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

“Nawasihi watanzania kuwa na subira ili uchunguzi ufanyike na tutahakikisha uchunguzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo na baada ya kukamilika wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria,” alisisitiza Masauni.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako alisema kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwanafunzi huyo ambacho kilitokea wakati wa kudhibiti maandamano yaliyokuwa yakifanyika katika eneo la Mkwajuni, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanafunzi Akwilina na anaungana na wazazi, familia, ndugu, jamaa na watanzania wote kuwapa pole za dhati kutokana na msiba huo,”alisema Ndalichako.

Aidha Ndalichako alibainisha kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itagharamia shughuli zote za mazishi ya mwanafunzi huyo na amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kusimamia shughuli zote za msiba huo.

Pia Ndalichako alitoa rai kwa watanzania kujiepusha na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusababisha maafa kwa watu wasio na hatia.

RAIS MAGUFULIA AMTUMBUA MKURUGENZI BUTIAMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Januari 23, 2018 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Butiama mkoani Mara Solomoni Ngiliule kuanzia leo kutokana na ubadhirifu wa fedha za Umma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo ametangaza maamuzi hayo leo zikiwa zimepita siku tatu toka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotoa maagizo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Waziri Mkuu aliagiza kiongozi huyo kuchunguzwa kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwemo sh. milioni 12 walizotumia kuandaa profile ya Halmashauri hiyo huku fedha zingine ni pamoja na sh. milioni 70 za elimu maalumu, sh. milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazikujulikani zimetumikaje.

Page 3 of 168