blog category

75000 WAFANYA MTIHANI KIDATO CHA 6

WATAHINIWA 74,920 leo wanaanza kufanya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Sita katika shule mbalimbali nchini huku watahiniwa 11,597 wakifanya mtihani wa Ualimu.

Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani (NECTA), John Nchimbi amesema kuwa mtihani wa kidato cha sita unaanza leo hadi Mei 19, mwaka huu.

Nchimbi amesema kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, watahiniwa 65,610 ni watahiniwa wa Shule huku watahiniwa wa Kujitegemea wakiwa 9,310.

Kwa upande wa mtihani wa ualimu, Nchimbi amesema kati ya watahiniwa 11,597 watakaofanya, watahiniwa 10,942 wanafanya Ualimu Daraja A na watahiniwa 654 wanafanya mtihani wa Stashahada ya Sekondari na mmoja anafanya Stashahada ya Ufundi.

Wafungwa Wanaosubiri Kunyongwa Magerezani Wafikia 465

Wafungwa Wanaosubiri Kunyongwa Magerezani Wafikia 465

IDADI ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa imekuwa ikiongezeka na hadi sasa imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo kutotekelezwa tangu mwaka 1994. Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mafunzo kwa waandishi wa habari mjini Morogoro jana, imebainisha kuwa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili kutekelezwa hadi Oktoba 2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi.

 Ripoti hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, imeonesha kuwa kuna mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

Wanaharakati

Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya, amesema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali kufuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo. Baadhi ya asasi zinazopinga kufutwa kwa hukumu ya kifo ni taasisi ya Under The Same Sun (UTSS), ambayo inasema katika utafiti waliofanya, wahusika wanataka hukumu hiyo hasa inayohusu watu walioua albino, itekelezwe mpaka hapo mauaji hayo yatakapokoma.

Hata hivyo, Mponezya amesema watetezi wengi wa haki za binadamu wanataka adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na kwa Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya wahukumiwa wamesubiri zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa, jambo linalowaathiri kisaikolojia.

Wananchi wagawanyika

Tume hiyo imekiri kwamba, Tanzania imeshindwa kutekeleza adhabu hiyo kwa miaka mingi kutokana na Serikali kueleza kuwa jamii imegawanyika kuhusu hukumu hiyo. Wapo wanaotaka ifutwe lakini wengi wanataka iendelee kutekelezwa kutokana na ongezeko la mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na albino.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mark Mulumbo, alipotakiwa kufafanua kuhusu mtazamo wa kisheria na kiserikali kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo katika mafunzo hayo, amekiri kwamba tafiti zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, kuna mgawanyiko kwa wananchi kuhusu adhabu hiyo.

Akifafanua zaidi, amesema hata katika mchakato wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hali hiyo ilijitokeza kwamba Watanzania wengi hawaoni kama muda ni mwafaka kufuta adhabu hiyo.

Marais

Kuhusu marais kushindwa kusaini hukumu hiyo, Mulumbo alisema upo mtazamo wa aina mbili kuhusu jambo hilo; wa kiimani na kisheria.

Amesema pamoja na kwamba nchi haina dini, marais wote waliowahi kuchaguliwa mpaka wa Awamu ya Tano, wana imani za kidini.

Wanaoipenda

Mwanasheria wa UTSS aliyewasilisha mada katika mafunzo hayo, Perpetua Senkoro, ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, amesema kwamba, utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa walemavu wa ngozi (albino) kuhusu hukumu hiyo, umeonesha jamii inataka iendelee kuwapo, na itekelezwe.

Senkoro amesema wana imani sawa na wanaharakati wenzao wa haki za binadamu kuwa dhana ya hukumu ni kumfanya mkosaji abadilike na hukumu ya kifo haitoi nafasi ya kubadilika, lakini kwao kutokana na namna wanavyouliwa kwa imani za kishirikina, hilo si suala la tabia bali ni imani na hivyo muuaji hawezi kubadilika, wanaona heri iendelee kuwapo na itekelezwe.

Pamoja na Tanzania kuridhia mapendekezo kadha wa kadha ya haki za binadamu, bado Mei 9 hadi 12 mwaka huu, katika mkutano wa Geneva, Uswisi itaulizwa utekelezaji wa mapendekezo mengine na msimamo wa nchi kuhusu kufuta adhabu ya kifo.

Mkutano huo utahudhuriwa na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu nchini, viongozi wa serikali pamoja na tume za haki za binadamu, ambapo nchi zaidi ya 190 zinatarajiwa kushiriki.

Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, imeonesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka 2015 katika utekelezaji wa hukumu ya kifo ni kubwa zaidi tangu mwaka 1990.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,634 waliuawa mwaka jana sawa na asimilia 50 ya waliouawa mwaka 2014. Aidha takwimu hizo hazihusu utekelezaji wa hukumu hiyo nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo huwa siri ingawa zinatajwa kuwa kubwa. Nchi zinazotajwa kutekeleza zaidi hukumu hiyo mwaka jana ni Iran, Pakistan na Saudi Arabia ambako asilimia 90 adhabu hiyo ilitekelezwa

TPDC KUTENGENEZA MADAWATI 500 AGIZO LA RAIS

Kutokana na agizo la serikali la kuzitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanakuwa na madawati ya kutosha katika shule zote za Msingi na Sekondari ambapo Halmashauri ya Wilaya ya mtwara imepewa ahadi ya kutengenezewa takribani madawati mia tano na kampuni ya TPDC

Akizungumza na Safari Redio Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Zacharia Nachoa amesema kuwa katika kusidiana na wahisani mbali mbali kampuni ya TPDC imehahidi kutoa takribani madawati mia tano

Akielezea mpango huo Nachoa amesema kuwa kutokana na zoezi lenyewe itakuwa ngumu TPDC kutengeneza madawati moja moja wakiwa Dar es salaam hivyo kutokana na mawasiliano ya mara ya mwisho TPDC wamesema watalazimika kutuma pesa hivyo Halmashauri ya Wilaya ya mtwara na wao watalazimika kutengeneza madawati hayo katika vituo vilivyopo katika kata na Manispaa hivyo wananchi watapata fursa ya kupata hiyo kazi

Sanjari na hayo Nachoa ameongeza kuwa Halmashauri nayo imepanga kutengeza takribani madawati mia nne na hiyo ni kutokana na kupata pesa kutoka katika mrahaba wa gesi vile vile kutoka na harambee ya mkuu wa wilaya imekuwa na matokeo mazuri hivyo itatumika ili kuhakikisha madawati yanapatika lakini pia wananchi nao wameanza kujitolea miti ya kupasua mbao ili kata zao zitengenezewe madawati

Wabunge Wa Upinzani Waja Na Staili Mpya Ya ‘Bunge Live’

Bungeni

Katika hali inayoonesha kutokata tamaa katika kuhakikisha wananchi wao wanasikia yale yanayoendelea Bungeni licha ya Bunge kutooneshwa ‘live’, wabunge wa upinzani wameibuka na mbinu mpya ya kurekodi sauti zao na yanayoendelea bungeni kwa kutumia simu zao na kisha kurusha sauti hizo katika mitandao ya kijamii na vituo vya redio vilivyopo katika majimbo yao.

Wabunge hao wa upinzani walifikia hatua hiyo baada ya wabunge wa CCM jana kuibuka kidedea pale walipowazidi wenzao wa upinzani kwa kura za sauti “siyooooo” kuikataa hoja ya kutaka matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja ‘live’ na televisheni.

Mbunge wa Malindi, Ally Salehe (CUF), ndiye aliyeibua hoja hiyo akitaka ufafanuzi wa kina kuhusu usitishwaji huo wa matangazo ya bunge ‘live’ huku akisisitiza kuwa uamuzi huo unakiuka Katiba ya nchi na haki ya kupata habari.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, Masoud Abdalla Salim (Mtambale-CUF), Rose Kamili (Viti Maalumu -Chadema), Ester Matiko (Tarime Mjini – Chadema) na Mussa Mbarouk (Tanga Mjini – CUF).

Salehe alizidi kudai kuwa matangazo ya Bunge yanarekodiwa kwa saa saba na kurushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) kwa saa moja tu, huku wabunge wa upinzani wakiondolewa na kuonyeshwa wa CCM pekee.

Hivi karibuni kumekuwa na hisia tofauti kutoka kwa wanasiasa, wananchi, vyama vya haki za binadamu na hata watu wa tasnia ya habari juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya bunge na badala yake bunge lenyewe litarekodi vipindi hivyo na kuvirusha usiku saa nne kupitia Televisheni ya Taifa (TBC).

MANISPAA MTWARA YALALAMIKIWA KWA UCHAFU

Wafanyabiashara wa samaki katika soko la feli manispaa ya mtwara mikindani mkoani mtwara wamelalamikia hali ya uchafu iliyokithiri katika eneo hilo la soko

Wakizungumza na mwandishi wa safari redio wafanyabiashara hao wamesema kuwa wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu kutokana na msongamano wa watu katika eneo hilo na hali hiyo ya uchafu iliyokithiri.

Mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina Seleman amesema kuwa wao kama wafanyabiashara wamekuwa wakilipa ushuru kwa usafi lakini hakuna jitihada zozote ambazo manispaa Imekuwa inazifanya kuhakikisha wanasafisha mazingira hayo na kuyaweka safi

katika hatua nyingine bw Seleman amesema kuwa katika soko hilo kuna kizimba ambacho kimejengwa maalumu kwa ajili ya kuhifadhi taka hizo lakini mpaka hivi sasa hakijaanza kutumika na kusababisha takataka kujaa katika eneo wanalozitupa mpaka kukaribia katika sehemu ambayo wanafanyia biashara ya samaki

baada ya malalamiko hayo safari redio ilitaka kuzungumza na viongozi wa soko hilo kwa upande wa serikali ili kutaka kujua serikali ina mipango gani kwa upande wa manispaa kuhakikisha soko hilo linakuwa safi na uongozi huo ulijibu kuwa wao sio wasemaji hawawezi kuzungumzia suala hilo zoezi la usafi ni agizo ambalo limetolewa na mheshimiwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania awamu ya tano Dk JOHN POMBE MAGUFULI katika sherehe za uhuru 9 desemba 2015 na kuzitaka halmashauri zote nchini kusimamia maeneo yake na kuayafanya yawe safi muda wote

Amuua Kaka Yake Baada Ya Kumfumania Akifanya Mapenzi Na Mke Wake

Mkazi wa Mahembo Manyanda Manyilizu,40, ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mdogo wake baada ya kumfumania akiwa na mkewe.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi amesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Mawemilu.

Kamanda Kisusi amedai mtuhumiwa na mwanamke walikimbia baada ya kufanya tukio hilo.

Katika tukio jingine, watu wawili wameuawa kwa kupigwa mawe na marungu kisha miili yao kuchomwa moto na wananchi katika tukio lilitokea juzi katika Kijiji cha Shimba wilayani Kahama.

Amesema watu hao walituhumiwa kuwa ni majambazi baada ya kumvamia Mchongaraji Ndalawa, 65, akiwa amelala nyumbani kwake wakimtaka awape fedha. Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama na hali yake inaendelea vizuri.

ZAIDI YA WATOTO 500 UFARIKI KILA MWAKA MKOANI LINDI

Takribani Watoto 314 walio chini ya umri wa miaka mitano pamoja na watoto wachanga 188 wanakadiriwa kupoteza maisha kila mwaka mkoani Lindi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vifaa tiba vya afya ya uzazi na mtoto.

Akizungumzia changamoto hiyo Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Lindi Dkt. Hussein Athuman amesema asilimia 50 ya vifo vya watoto wachanga vinatokana na ukosefu wa vifaa tiba, huku Dkt.John Rojas kutoka shirika la EGPAF linalosaidia afya ya uzazi akisema hali bado hairidhishi katika eneo hilo.

Dkt John amesema serikali na wadau hapa nchini wanatakiwa kushirikiana na kuongeza nguvu za ziada katika kupambana na vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa kuweka mipango mbalimbali ikiwemo kuongeza vifaa tiba katika vituo vya afya.

Akiongea wakati wa kukabidhiwa vifaa tiba Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi amelishukuru shirika la EGPAF kwa kutambua umuhimu wa wananchi na kuyataka mashirika mengine kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na vifo dhidi ya wanawake wajawazito na watoto.

Zambi amepokea vifaa tiba kwa ajili ya wakina mama wajawazito na watoto wachanga vitakavyosambazwa katika vituo vya afya 54 na vifaa vilivyopokelewa ni pamoja na vile vya kumsaidia mtoto kupumua vizuri, na vitanda vya kujifungulia, msaada huo umetolewa na shirika la EGPAF kwa msaada wa watu wa Marekani.

Serikali Ya Dkt. Kikwete Haikukomba Fedha Hazina-Dkt. Mpango

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete haikukomba fedha katika Hazina kama ambavyo baadhi ya wabunge wamedai na kudai kuwa hata Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), lilifanya tathmini na kutoa taarifa safi.

Dkt. Mpango ameeleza hayo bungeni wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia mjadala wa wizara mbili zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Utawala Bora, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge wamesema Serikali ya Awamu ya Nne ilikomba fedha zote Hazina na kusababisha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John Magufuli kukuta Hazina haina fedha.

Akijibu hoja hiyo, Dkt. Mpango amesema hakuna ushahidi ulioitia hatiani Serikali ya Awamu wa Nne kuhusu kukomba fedha Hazina na kwamba IMF na wadau wengine wa kimataifa, walifanya tathmini huru ya bajeti na mwenendo wa uchumi nchini na taarifa yao ya mwisho waliitoa Desemba, 2015.

Katika ripoti hiyo hakuna mahali ilipoonesha nchi ilikuwa na hali mbaya ya fedha na kwamba kwa kudhihirisha hilo, vigezo vya kimataifa vilionesha bayana kuwa Deni la Taifa ni himilivu na nchi bado inakopesheka na imeendelea kulipa mishahara watumishi wake pamoja na madeni mengine bila kutetereka.

Amesema Serikali iliendelea kulipa madeni mengi na hakuna kilicholegalega, huku ikiendelea pia kugharimia shughuli za mihimili yote, ikiwemo Bunge, usalama wa nchi na kuendelea kulipa madai ya makandarasi na watoa huduma wengine.

Page 165 of 168