blog category

WAZIRI MKUU AMEWATAKA WAFANYABIASHARA KUTUMIA TAASISI ZA KIFEDHA KUKUZA MITAJI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wilayani Ruangwa kutumia taasisi za kifedha kukopa fedha kwa ajili ya kukuza mitaji yao.

Ameyasema hayo jana Jumapili, Machi 25, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa wilaya hiyo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Walimu, wilayani Ruangwa.

Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema ni vema wakatumia taasisi za kifedha zilizopo ili kukuza mitaji yao.

Amesema katika kuhakikisha riba zinapungua, Rais Dkt. John Magufuli anaendelea kuzungumza na wamiliki wa taasisi za kifedha ili waone namna ya kupunguza riba hiyo.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali la kuchukua hatua hiyo ni katika kutekeleza mkakati wake wa kuwawezesha wafanyabiashara ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu.

Pia Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali ipo pamoja nao na imedhamilia kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama maji na afya.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Said Shea amewaomba wafanyabiashara wenzake watumie fursa za maendeleo zilizoko wilayani humo kwa kupanua wigo wa biashara zao.

KAMATI YA KITAIFA YA UN NA SERIKALI ZA KETI

Kamati ya kitaifa inayoendesha mradi wa pamoja kati ya mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa (UNESCO, UN Women na UNFPA) na serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wizara nyingine ambazo zinahusika na maswala ya Elimu hususani TAMISEMI, Wizara ya Afya, Maedeleo ya Jamii, Jinsia, Watu Wazima na Watoto na Wizara ya Sheria na Katiba pamoja na mfadhili wa mradi KOICA imekutana kwa mara yake ya kwanza kujadili mwelekeo wa mradi unawo husu kumwendeleza msichana na mwanamke kijana kupitia elimu.

Mkutano huo uliokuwa chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo umeangalia na kubadilishana mawazo ya hatua zilizofikiwa katika mradi huo ulioanza mwaka 2016 na kutekelezwa katika wilaya nne nchini Tanzania (Kasulu, Ngorongoro, Sengerema na Mkoani, Pemba) kwenye kata 22 na kupitia mpango wa mwaka 2018.

Akizungumza kabla ya kusimamia mazungumzo, Dk Akwilapo amewashukuru wafadhili na pia wadau wengine waliojipanga kufanikisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya wanawake nchini Tanzania na uchumi kwa ujumla.

Amesema wizara hizo zimekuwa zikifanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba taifa linatoa elimu yenye ubora na kusaidia wale waliopo pembezoni wanapata elimu hasa wasichana na wanawake vijana ambao hawako shuleni kwa sababu mbalimbali.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa UNESCO Kanda ya Afrika Mashariki, Viola Kubaisa amesema kwamba mkutano huo wa mashauriano kwa mradi huo unaoendeshwa Ngorongoro, Mkoani Pemba, Kasulu na Sengerema ni muhimu kwa kuwa unapanga mpango kazi na kuangalia namna bora ya utekelezaji wa mradi huo.

ABDUL NONDO AACHIWA KWA DHAMANA

Leo March 26, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemuachia kwa dhamana Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania Abdul Nondo ambaye alikuwa anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Iringa.

Nondo amepewa masharti ya dhamana ni wadhamini wawili mmoja mtumishi wa Serikali wote wakazi wa Iringa na bondi ya kauli Tshs Milioni 5, atarudi Mahakamani April 10, 2018.

Nondo anashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni March 7 ya mwaka huu kuwa maisha yake yapo hatarini akiwa katika eneo la Ubungo na kuzisambaza kwenye mtandao wa Whatsapp.

Kosa la pili limetajwa kuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga wakati alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha polisi mjini humo kwa kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

TANZANIA KUPATIWA MAFUNZO MAALUM ISRAEL

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema Tanzania inatarajia kupeleka wataalamu wake wa masuala ya intelijensia nchini Israel kwa ajili ya kupatiwa mafunzo maalumu.

Dkt. Mwimyi amezungumza hayo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kumpokea Waziri wa Ulinzi wa Taifa ka Israel Avigdor Liberman na kusema wamekubaliana kuhakikisha wanaimarisha mambo yakiusalama ndani na nje ya nchi hizi mbili na kubadilishana mbinu mpya za kupambana na wahalifu hata kwa zile njia ambazo ni ngumu kufikia katika hali ya kawaida.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israel Avigdor Liberman amesema uhusiano wa nchi hizi mbili ni mkubwa na wamuda mrefu ndio maana wameamua kuleta tekinolojia za kiusalama ili kuilinda Tanzania na wahalifu sambamba na hapo wataendelea kutoa ushirikiano wao kwa ujuzi na ugunduzi wa tekinolojia mbalimbali hasa zinazohusiana na usalama wa nchi.

RAIS MAGUFULI KUZINDUA MAGARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Machi 26, amepokea na kuzindua magari 181 ambayo yatakuwa yakitumika kusambaza madawa vijijini na mjini.

Rais Magufuli ndiye alikuwa mgeni rasmi na kuzindua magari hayo 181 yaliyopo chini ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Katika uzinduzi huo Rais Magufuli amewapongeza wafanyakazi MSD kwa kazi nzuri wanayo ifanya katika jamii.

Aidha amewataka wawekezaji na wizara ya Afya kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kujenga viwanda vya utengenezaji wa vifaa tiba.

WAZIRI MKUU ASAINI MKATABA WA UWANZISHWAJI WA SOKO LA PAMOJA KATIKA UMOJA WA AFRIKA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepongeza makubaliano yaliyofikiwa na nchi za Afrika za kulifanya bara hilo kuwa eneo huru kibiashara.

Majaliwa aliyasema baada ya kumaliza kusaini mkataba wa nchi za Afrika kuhusu mkataba huo akimwakilisha Rais John Magufuli Jijini Kigali ambapo alisema Tanzania imeajiandaa vya kutosha kutekeleza mkataba huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali , Waziri Mkuu alisema Tanzania itahakikisha mkataba huo unatelekezwa bila kuathiri huduma zinazozalishwa ndani.

Alisema Tanzania itahakikisha mikataba mitatu ambayo imesainiwa inatekelezwa bila kuathiri uzalishaji na sera za ndani.

Mikataba iliyosaioniwa na mataifa hayo 50 ya Bara la Afrika ni pamoja na mkataba wa kulifanya bara la Afrika kuwa eneo huru la biashara, Itifaki ya kisheria ya utekelezaji wa makubaliano hayo ikiwamo uhuru wa makazi, haki ya kuishi na kufanyakazi popote bila vikwazo wala vizuizi vyoyote.

Azimio la tatu ni Azimio la Kigali ambalo limejumuisha mawazo ya uanzishwaji wa mchakato huo.

Vile vile katika uhuru wa biashara ya anga ambapo Tanzania bado tuna ndege chache ili tusije kuruhusu kiholela, l;azima tuwe waangalifu katika hilo.

Awali akihutubia katika ufunguzi wa sherehe hizo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliyataja maeneo makuu ambayo mkataba huo umeangazia kuwa ni pamoja na eneo huru la biashara ya anga, miundombinu ya reli na barabara ambayo itaziunganisha nchi za Afrika kuwasiliana kwa urahisi.

Mkataba huo ulisainiwa jana baada ya vikao vya maadalizi vilivyohusisha timu za wataalam na mawaziri wa biashara na mambo ya nje ya nchi zinazounda Umoja huo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 50 wanachama wa AU ambao walisaini mkataba huo.

ESRF WAPONGEZWA KUPITIA SIDP

Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), imepongezwa kwa kazi zake inazofanya za utafiti na kutoa mwelekeo sahihi wa uanazuoni kwenye masuala mazito yanayotakiwa kutekelezwa na wananchi wa Tanzania kuendeleza ustawi na kuinua uchumi.

Aidha imepongezwa kwa kurejea kuipitia sera ya maendeleo endelevu (SIDP) ya mwaka 1996 ambayo kwa sasa inahitaji kufanyiwa marekebisho kuendena na maizngira ya sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof Elisante Ole Gabriel, katika hotuba iliyosomwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda wa Wizara hiyo, Obadiah Nyagiro wakati akifungua mkutano wa tano wa wajumbe wa kitaifa wakiwemo wataalamu wa kupitia sera na maeneo maalumu yanayogusa maendeleo (NRG5) ambapo walijadili sera ya maendeleo endelevu ya viwanda: Nini Nafasi ya usalama wa chakula, hali ya hewa na biashara?

Amesema kwamba majadiliano hayo yanakwenda sawa na juhudi za serikali ya awamu ya tano ya kujikita katika maendeleo ya viwanda ambapo uwekezaji na biashara ni vitu muhimu.

Amesema mwaka 1996 serikali ya Tanzania ilizindua sera ya maendeleo endelevu (SIDP) ikiwa imepangwa kuibeba nchi kuanzia mwaka huo hadi mwaka 2020.

Lengo ya sera hiyo ni ilikuwa kuiweka Tanzania katika njia ya viwanda na kufikia malengo ya kitaifa kama ilivyoelezwa katika malengo ya taifa (TDV) kufikia 2025.

Alisema kwa miaka mingi utekelezaji wa SIDP umekuwa ukisaidiwa na sera mbalimbali za kilimo, fedha na biashara na mikakati ya maendeleo.

Kuelekea katika viwanda kunakwenda sanjari na kuangalia mipango ya maendeleo ingawa kuna hisia kwamba suala la usalama wa chakula mabadiliko ya hali ya hewa na usindikaji wa mazao ya kilimo yamekuwa yakiachwa katika kuongeza uimara wa safari ya maendeleo.

Mapungufu yaliyopo ndani ya SIDP yanahitaji kuangaliwa ili kutoa umuhimu wa kuunganisha masuala hayo muhimu ambayo ni mtambuka na maendeleo ya viwanda.

Kwa kuunganisha masuala hayo na kuangalia jinsia taifa litakuwa na sera bora kabisa ya viwanda yenye kubeba kila kitu kinachotakiwa katika kuelekea uchumi unaotegemea viwanda na kujali mazingira.

Amesema kutokana na mazingira hayo ni dhahiri kwamba mkutano huo na maazimio yake yatakuwa chachu kwa watengeneza sera ambao wanatakiwa kuipitia sera hiyo na kuipa uhai mpya.

Naye Mkuu wa Idara ya Utafiti na Machapisho wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene aliyesoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dk Tausi Kida akikaribisha wajumbe wa mkutano huo, alisema kwamba mkutano huo mkubwa wa kitaifa umelenga kutoka na maazimio ambayo yatasaidia watunga sera kuihuisha sera iliyopo na mikakati mbalimbali ya kuipeleka Tanzania katika dunia ya viwanda.

Alisema mkutano huo unafanana na ule uliofanyika Agosti 24 mwaka jana ambao uliangalia mambo mbalimbali yanayohusiana na sera hiyo na kuihusisha katika SIDP.

Alisema haja ya kuangalia sera hiyo kunatokana na ukweli kuwa kuna mapengo kadha katika sera yanayosababisha ufanisi mdogo wenye tija katika uchumi na biashara pia katika kilimo.

Upitiaji huo wa SIDP umefanywa na ESRF kwa kufadhiliwa na CUTS International na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Washiriki pia walipata nafasi ya kupewa taarifa ya hali ya kilimo nchini na majadiliano ya masoko kupitia Shirika la Biashara Duniani (WTO) na taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia na mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC).

Katika mkutano huo mada mbalimbali ziliwasilishwa zilizoangalia sekta mtambuka zikiwamo za kilimo na viwanda.

MVUA YASABABISHA KUKATIKA KWA BARABARA YA ITIGI

Mvua kubwa iliyonyesha katika eneo la Nyahua wilayani Uyui Mkoani Tabora imesababisha kukatika kwa barabara kuu ya Tabora kupitia Itigi hadi Dodoma na kusababisha magari ya abiria na mizigo kwishindwa kuendelea na safari zake kwa kutumia barabara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze amesema mvua zilizonyesha katika maeneo hayo zimesababisha kukatika kwa eneo hilo ambapo ndipo barabara ya lami inaishia.

Amewataka madereva wa magari ya aina yoyote kudiriki kupita katika aina hilo kwa sababu wanaweza kuhatarisha maisha yao na abiria na mizigo.

Ndabalinze amesema dereva yoyote atakayekaidi na kuamua kupita katika eneo hilo kwa kulazimisha jambo lolote litakalompata itakuwa ni yeye kajisababishia na asilelekeze lawama kwa chombo chochote.

Amesema wakati taratibu nyingine zikiendelea za kutaka kurejesha mawasiliano kwa kutumia barabara hiyo ni vema magari yote ya kuja na kutoka Tabora yakapitia barabara ya Manyoni , Singida , Nzega hadi Tabora.

Naye Afisa Mfawidhi wa SUMTRA Mkoa wa Tabora Joseph Michael amesema kutokana na tatizo la kukatika kwa barabara hiyo anatoa ruhusa kwa magari yote yaliyokuwa yakipitia barabara ya Tabora kupitia Itigi hadi maeneo ya Dodoma na Dar es salaam kuzungukia Nzega bila kibali.

Page 1 of 168